
Ripoti ya Umoja wa Mataifa, imebaini kuwa wanajeshi wa Uganda waliopo nchini Sudan Kusini, wamekuwa wakiwalenga raia wa kawaida katika taifa hilo linaloendelea kushuhudia changamoto za kiusalama na kisiasa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika ripoti iliyochapishwa Februari tarehe 27, Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, imevishtumu vikosi vya Uganda ambavyo vinashirikiana na vile vya wenyeji na kuwauwa raia wa kawaida.
Umoja wa Mataifa unasema, vikosi vya Uganda vimekuwa vikisaidia vile vya Sudan Kusini kushambulia makaazi ya watu wa kawaida na kuharibu makaazi yao.
Hata hivyo, jeshi la Uganda limekanusha madai hayo, kwa kueleza kuwa katika historia yake ya miaka 45, haijawahi kuwalenga raia wa kawaida.
Aidha, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imesema, uwepo wa vikosi vyake nchini Sudan Kusini, umesaidia pakubwa kuhakikisha nchi hiyo inakuwa tulivu, hasa usitishwaji wa vita jijini Juba.
Tangu mwezi Machi mwaka 2025, jeshi la Uganda limekuwa jijini Juba baada ya ombi la rais Salva Kiir, baada ya kushuhudia upinzani kutoka kwa vikosi upinzani chini ya aliyekuwa Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.