
Ndege ya kijeshi ya Marekani ya kubeba mafuta ya ndege iliyoshiriki katika operesheni dhidi ya Iran imeanguka nchini Iraq. Shughuli za uokoaji zinaendelea, kamandi kuu ya Marekani (CENTCOM) imetangaza siku ya Alhamisi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Haijulikani bado kama kuna majeruhi wowote. Afisa wa Marekani, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa shirika la habari la Associated Press ili kutoa maoni kuhusu hali hiyo, amebainisha kwamba ndege ya KC-135 iliyoanguka ilikuwa na wafanyakazi watano.
Ajali hiyo haikusababishwa shambulizi kutoka kwa adui au kwa rafiki, jeshi limesema katika taarifa, likielezea ndege hiyo kama “hasara kubwa.”
CENTCOM, ambayo ni kamandi ya jeshi la Marekani Mashariki ya Kati, imesema ndege mbili zilihusika: moja ilitua salama huku nyingine ikianguka magharibi mwa Iraq.
Afisa mwingine wa Marekani, pia akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amebainisha kwamba ndege nyingine KC-135 iliyohusika pia ilikuwa ya kubeba mafuta ya ndege.
“Taarifa zaidi zitatolewa kadri hali inavyoendelea,” CENTCOM imesema. “Tunaomba uvumilivu wenu tunapokusanya taarifa zaidi na kutoa ufafanuzi kwa familia za wanajeshi.”
Ndege hii ya kubeba mafuta ya ndege ni ndege ya nne kutambuliwa rasmi kuwa imeanguka wakati wa operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran. Wiki iliyopita, ndege tatu za kivita za Marekani zilidunguliwa kimakosa na makombora kutoka kwa mshirika Kuwait.
Wafanyakazi sita wa ndege ya F-15E Strike Eagles waliondoka salama salimini na wako katika hali nzuri baada ya kuondoka ndani ya ndege hiyo, Marekani iliripoti.
Wanajeshi saba wa Marekani wameuawa vitani tangu kuanza kwa vita dhidi ya Iran, na takriban 140 wamejeruhiwa, wakiwemo wanane vibaya, Pentagon ilitangaza mapema wiki hii.
Rais Donald Trump na Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth wote wameonya kwamba vita dhidi ya Iran huenda vikasababisha vifo vya Wamarekani wengi zaidi kabla ya kumalizika.
Wanajeshi sita waliofariki waliuawa wakati ndege isiyo na rubani ya Iran iliposhambulia kituo cha operesheni katika bandari ya raia huko Kuwait. Walikuwa wanajeshi wa akiba waliokuwa wakifanya kazi katika usafirishaji, wakiwapa wanajeshi chakula na vifaa.
Walifariki siku moja baada ya uzinduzi wa mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, mnamo Februari 28. Jamhuri ya Kiislamu imejibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel na mataifa kadhaa ya Ghuba ya Kiarabu yanayowahifadhi wanajeshi wa Marekani.
Mwanajeshi wa saba wa Marekani amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio la Machi 1 kwenye Kituo cha Jeshi la Anga cha Prince Sultan nchini Saudi Arabia.
Rais Trump alijiunga na familia zinazoomboleza kwa sherehe ya kuaga wapendwa wao katika kituo cha Jeshi la Anga cha Dover huku miili ya wanajeshi sita wa kwanza ikirudishwa makwao. Makamu wa Rais JD Vance, Jenerali Hegseth, na watu wengine mashuhuri walitoa heshima zao kwa gari la kubeba maiti lililofunikwa na bendera lilipowasili Dover wiki hii.