Diwani wa Kata ya Chanika wilayani Handeni Mkoani Tanga, Dkt. Habibu Mbota, ametoa msaada wa sadaka kwa wajane na wazee wa kata hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea sikukuu ya Eid, akilenga kuwafariji na kuwasaidia kupata mahitaji muhimu ya sikukuu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Dkt. Mbota amesisitiza umuhimu wa watu wenye uwezo kuwasaidia majirani na wahitaji katika jamii, akieleza kuwa kipindi cha Mfungo wa Ramadhani kinapaswa kuwa chachu ya kuimarisha upendo, mshikamano na kusaidiana.
Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha watu wanaowazunguka wanapata angalau chakula cha kusherehekea sikukuu, hasa makundi yenye uhitaji kama wajane na wazee.
Sambamba na hilo, Dkt. Mbota ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuiombea dunia amani, akieleza kuwa zipo nchi ambazo hazipotezi watu kwa magonjwa bali zinapoteza familia kutokana na vita.

(Feed generated with FetchRSS)