Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran, Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi amesema kambi za kijeshi za Marekani zilizoundwa kwa kutumia rasilimali za Waislamu kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa eneo, huku zikifuja mali za mataifa ya Waislamu, zimeharibiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Brigedia Jenerali Shekarchi amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Fars na kuongeza kuwa, makamanda na wanajeshi wa Marekani waliokuwa katika kambi hizo wameuwa au kujeruhiwa katika hujuma hizo za kisasi za Iran.

Ameeleza bayana kuwa, Marekani si dola lenye nguvu na ushawishi tena duniani, na kusisitiza kuwa vikosi vamizi na vya kigaidi vya nchi hiyo vinapasa kufukuzwa katika eneo la Asia Magharibi.

Msemaji wa Majeshi ya Iran huku akizihutubu nchi za Kiislamu amesisitiza kuwa, “Msiamini kile kinachoelezwa kuwa nguvu na uwezo wa Marekani, uwezo ambao hauwezi hata kulilinda jeshi lake linalofifia.” Amewaasa viongozi wa Waislamu katika eneo kuungana dhidi ya ‘ukafiri, ushirikina, na unafiki’ ambao unaongozwa na Marekani na Wazayuni.

Kadhalika Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran ameashiria kuhusu meli ya kijeshi ya kubebea ndege za kivita ya Marekani ya Abraham Lincoln na kubainisha kuwa: Manowari kubwa zaidi ya kivita ya Marekani, ambayo wakati fulani ilitoa motisha kwa ugaidi na kufyonza mali za Waislamu, ilidumazwa na Jamhuri ya Kiislamu na kulazimika kurejea nyuma, katika kushindwa na pigo ambalo litaandikwa katika madaftari ya historia.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) linaendeleza wimbi la mashambulizi makali ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4 dhidi ya kambi na maslahi ya adui Mmarekani na Mzayuni katika eneo la Asia Magharibi. 

Vita hivi  vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea kuwa tata zaidi na vya umwagaji damu kadiri siku zinavyosonga, huku adhabu dhidi ya wavamizi ikiendelea kubaki katika ajenda kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran.

Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Majeshi ya Iran amesema, “Iran inaweza ikakarabati kile kilichoharibiwa katika mashambulizi ya Marekani na Israel, lakini kile ambacho hakiwezi kurekebishwa ni itibari ya Marekani, nguvu zake hewa, jeshi lake lililoshindwa, na utawala wa Kizayuni uliochakazwa.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *