Marekani. Mtoto wa marehemu mfalme wa muziki wa pop, Paris Jackson, ni mmoja wa watoto waliokulia katika familia yenye umaarufu mkubwa duniani. 

Akiwa mtoto wa Michael Jackson, maisha yake yamekuwa yakivutia macho ya watu tangu akiwa mdogo.

Paris  alizaliwa Aprili 3, 1998 nchini Marekani na kukulia katika familia ya wasanii maarufu. Umaarufu wa baba yake ulimfanya aishi maisha ya kistaa.

Ikumbukwe Michael Jackson alifariki dunia mwaka 2009 baada ya kifo hicho Paris pamoja na ndugu zake walilelewa na bibi yao, Katherine Jackson, ambaye alisimamia ukuaji wao.

Mikiki imekuchambulia maisha yake, kazi zake za sanaa pamoja na kashfa mbalimbali za kutumia madawa ya kulevya.
Njia yake

Tofauti na matarajio ya watu kuwa huenda mtoto huyo angerithi mikoba ya baba yake MJ mambo yamekuwa tofauti na amejichaguliwa njia yake mwenyewe.

MJ alikuwa muimbaji wa muziki wa Pop lakini Paris aliingia kwenye muziki wa mtindo wa Indie na Rock ambao hakuna mwanafamilia yeyote aliyewahi kuufanya.

Mbali na muziki Paris ana vipaji vingi amewahi kuigiza kwenye filamu mbalimbali za Marekani miongoni mwa kazi hizo ni Gringo ya mwaka 2018 akicheza kama Nelly, The Space Between, Habit, Sex Appeal na One Spoon of Chocolate.

Lakini pia ni mwanamitindo maarufu nchini humo akifanya kazi na kampuni ya IMG Models inayowasimamia walimbwende wakubwa nchini Marekani.

Tangu aanze kazi ya usanii mwaka 2010 ameachia albamu moja iitayo ‘Wilted’ akiitoa mwaka 2020 chini ya lebo ya Republic lakini ameachia Extended Playlist (EP) mbili tu.

Moja inaitwa The Lost EP aliyoiachia mwaka 2022 na nyingine The Soundflowers ya mwaka 2020 chini ya lebo ya Self Released.
Ingawa amefanya kazi hizo lakini wakosoaji wanasema Paris sio mzuri kwenye kuimba kama alivyo baba yake lakini akikaa kwenye kamera kuigiza anatisha zaidi.

Wengi wanaamini mwanadada huyo anapita na upepo wa jina la baba yake na sio kwamba ana kipaji halisi kama ilivyokuwa familia yao ambayo kuanzia baba yake shangazi zake wote walikuwa wasanii waliounda kundi la The Jackson 5.

Alichorithi

Licha ya kujenga maisha yake binafsi, Paris Jackson bado anaonyesha heshima kubwa kwa baba yake na urithi wa muziki wa mfalme huyo wa Pop.

Mara nyingi amekuwa akishiriki katika matukio ya kumbukumbu ya Michael Jackson na kuelezea jinsi baba yake alivyomsaidia kumfikisha hapo alipo.

Kwa ujumla, Paris ameendelea kuonyesha kuwa licha ya kubeba jina kubwa la familia ya Jackson, ana uwezo wa kujenga brandi yake kama msanii.

Licha ya ukaribu huo, kumewahi kuripotiwa kuhusu migogoro ya mara kwa mara kuhusu urithi na usimamizi wa mali za baba yake Michael.

Migogoro hiyo imewahi kuhusishwa na baadhi ya wanafamilia wa Jackson ambao wamewahi kujaribu kuwadhulumu watoto hao ingawa mara kadhaa Paris amekuwa akiepuka kuzungumzia.

Hivi karibuni Paris amewahi kuwa kwenye uhusiano na wanamuziki na watu wa tasnia ya burudani.

Miongoni mwa mahusiano yaliyowavutia mashabiki ni ule aliotoka na mwanamuziki Gabriel Glenn. Wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja katika bendi yao ya The Soundflowers, kabla ya kuachana mwaka 2020.

Paris pia aliwahi kuhusishwa kimapenzi na mwanamitindo na mwigizaji wa Uingereza Cara Delevingne. Ingawa hawakuwahi kuthibitisha rasmi uhusiano wao, ukaribu wao uliwahi kuwa gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Paris amewahi kuzungumzia kuwa kuishi kwenye familia ya watu maarufu ilikuwa changamoto kubwa kwake mwanzoni lakini baadae alizoea.

“Kuna muda unahitaji usiri au kuwa faragha na familia yako au hata marafiki ukitokea tu mara ushapigwa picha kesho umesambaa magazetini unakuwa hauna uhuru wa kutoka.” Anasema Paris

Anasema mbali na changamoto hiyo aliwahi kupata msongo wa mawazo kutokana na presha kubwa na matarajio makubwa kutoka kwenye vyombo vya habari.
Madawa

Mwanadada huyo  amewahi kuhusishwa na matumizi ya dawa za kulevya katika baadhi ya ripoti za vyombo vya habari, hasa alipokuwa akipitia changamoto za kisaikolojia baada ya kifo cha baba yake.

Mwenyewe amewahi kukiri katika mahojiano kadhaa kuwa aliwahi kupitia kipindi kigumu akiwa kijana, na alijaribu kutumia baadhi ya vitu kama pombe kupita kiasi na dawa za kulevya. Hata hivyo, alieleza kuwa hali hiyo ilitokana na msongo wa mawazo, upweke na presha ya maisha ya umaarufu.

Anasema hata hivyo vitu hivyo havikumsaidia kuwa sawa na mara kadhaa amewahi kuzungumzia kuhusu changamoto alizopitia ili kuhamasisha vijana kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na kutunza afya ya akili.

Utakumbuka baba yake amewahi kuhusushwa na kashfa ya kuwalawiti watoto wadogo ambao alikuwa akiwaalika kila wikiendi nyumbani kwake.

Paris amewahi kuzungumzia suala la ubakaji na katika baadhi ya mahojiano yake aliwahi kubakwa akiwa bado mdogo na mzee ambaye hakuwahi kumtaja.

Anasema tukio hilo lilikuwa moja ya mambo yaliyomletea maumivu makubwa ya kihisia na kuchangia changamoto za afya ya akili alizopitia wakati wa ujana wake.

Paris anasema kuwa kwa muda mrefu alibeba maumivu hayo kimya kimya kabla ya kuamua kuzungumza hadharani ili kusaidia wengine wanaopitia hali kama hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *