Mashabiki wa timu ya taifa ya England watalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kununua jezi zitakazotumika na timu hiyo katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kutangazwa kwa bei yake ambayo itakuwa ndio ghali zaidi duniani katika historia.

Baada ya ongezeko la bei ambalo ni karibu mara mbili ya kiwango cha mfumuko wa bei, jezi ya mechi kwa watu wazima inauzwa kwa bei kubwa ya Pauni 134.99 (Sh463,879), ikiwa ni ongezeko la asilimia nane ukilinganisha na jezi kama hiyo iliyotolewa kabla ya Euro 2024 ambayo ilikuwa Pauni 124.99 (Sh429,516).

Hata mashabiki vijana watalazimika kulipa zaidi ya Pauni 100 (Sh343,640) ili kuvaa jezi ya mechi, huku jezi za watoto zikiuzwa kwa bei ya juu ya Pauni 114.99 (Sh395,152).

Wakati huo huo, jezi ya watu wazima ya uwanjani imeongezwa kwa asilimia sita na kufikia Pauni 89.99 (Sh309,242), huku toleo la watoto likiwa na bei ya Pauni 69.99 (Sh240,514).

Jezi ya mechi inafanana zaidi na ile inayovaliwa na wachezaji wa England wakati wa mashindano, ilhali jezi ya uwanjani imeundwa kwa ajili ya mashabiki kuvaa kwa matumizi ya kawaida wanapokuwa uwanjani.

Mashabiki watakaochagua kuweka jina na namba mgongoni watalazimika kulipa hadi Pauni 60 (Sh206,183) za ziada.

Jezi ya mechi ya England iliuzwa kwa Pauni 114.95 (Sh395,014) kabla ya Kombe la Dunia la 2022, huku jezi ya uwanjani ikigharimu Pauni 74.95 (Sh257,558).

Jezi hiyo imetengenezwa na kampuni ya Nike kama sehemu ya mkataba unaoripotiwa kuwa wa Pauni 400 milioni (Sh1.4 trilioni) kati ya kampuni hiyo ya vifaa vya michezo na Chama cha Mpira wa Miguu England (FA).

Tofauti na hapo awali, jezi hiyo haina tena muundo wa rangi nyingi wa Msalaba wa St George uliosababisha malalamiko na mjadala ilipotolewa mwaka 2024.

Badala yake, msalaba huo umeondolewa na kuwekwa maneno “happy and glorious” ndani ya kola, yakitoa heshima kwa wimbo wa taifa wa England “God Save the King”.

Nike imeielezea jezi hiyo kama “muundo wa kisasa wa rangi nyeupe unaoheshimu urithi wa England”, huku jezi ya ugenini ikirejea kuwa nyekundu baada ya kuwa ya rangi ya zambarau tangu mwaka 2024.

Jezi hizo zimewekwa hadharani kupitia taarifa iliyotolewa kwenye tovuti rasmi ya FA ikitangaza uzinduzi wa jezi hizo mpya siku ya Jumatatu.

“Katika maandalizi ya Kombe la Dunia la FIFA 2026, England imetoa video yenye mvuto kuonesha muundo wa jezi mpya za nyumbani na ugenini za Three Lions.”

Timu ya England itacheza dhidi ya Uruguay Ijumaa hii kisha kukutana na Japan Jumanne ijayo, huku michezo yote ikiwa ya kirafiki.

Jezi hiyo mpya inatarajiwa kuvaliwa kwa mara ya kwanza na England siku ya Ijumaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *