RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na uongozi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) uliofika Ikulu, Zanzibar, leo Machi 30, 2026.
Ujumbe huo ulioongozwa na Rais wa chama hicho, Dk. Mary Mwanyika Sando, uliwasilisha dhamira ya kuandaa Mkutano Mkuu wa Vyama vya Madaktari Wanawake Afrika unaotarajiwa kufanyika Zanzibar Mei 5, 2027. Mkutano huo unatarajiwa kuwashirikisha madaktari takriban 400 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika. SOMA: Mkumbo: Changamkieni matibabu bure

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Mwinyi amesema kufanyika kwa mikutano ya kimataifa nchini ni tija kubwa na fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar kimataifa pamoja na kuimarisha sekta ya utalii. Amesema washiriki wa mikutano hiyo huwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar wanaporejea katika nchi zao.
Aidha, Dk. Mwinyi amepongeza juhudi za MEWATA kwa kuamua kuandaa mkutano huo Zanzibar, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya na uchumi kwa ujumla. Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kushirikiana na MEWATA kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mkutano huo unafanikiwa kwa kiwango cha juu.