
Mbeya City imetenga Sh10 milioni kwa wachezaji ili kuwahamasisha waibuke na ushindi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC kesho, Ijumaa, katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Manyara.
Katibu Msaidizi wa Mbeya City, Joseph Mlundi amesema lengo la kutenga kiasi hicho ni kuongeza morali kikosini.
“Japokuwa ndio kawaida yetu kutoa bonasi kwa wachezaji wanaposhinda au kutoa sare lakini kwa mchezo huu na KMC huenda hali ikabadilika zaidi kwa kuwa Mmurugenzi wa Jiji ametangaza kwa ujumla”
“Kawaida haipungui Sh 5 milioni ila kwa hii itafika hadi Sh 10 milioni, lengo ni kuwapa motisha vijana kupigania nembo ya Jiji la Mbeya tunaamini kuanzia mechi hiyo City haitakamatika,” alisema Mlundi.
Beki wa timu hiyo, David Mwasa, alisema wanafahamu ugumu wa mchezo huo kutokana na hali ya wapinzani wao, lakini kwa matokeo waliyonayo hawana sababu ya kukosa pointi tatu muhimu.
“Tunajua mechi itakuwa ya ushindani kwa kuwa kila mmoja anataka pointi tatu, niwaombe mashabiki kutuombea na kutusapoti na sisi wachezaji tutapambana kubaki salama Ligi Kuu, tuko tayari kwa kila mchezo,” amesema Mwasa. Mbeya City inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.