
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu la Zanzibar (ZFF) linahitaji jumla ya Sh1.2 billioni kwa ajili ya mashindano ya ligi ya Muungano yanayaotarajiwa kuanza Aprili 21 hadi 27 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai alisema mashindano hayo yatashirikisha timu nane ikiwa ni nne kutoka Bara na nne za Zanzibar.
Timu hizo ni mabingwa watetezi Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars wakati kutoka Zanzibar ni ni KVZ, Muembe Makumbi, Mlandege na Mafunzo.
Vuai alisema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya zawadi za washindi, zawadi mbalimbali za kila mechi kama mchezaji bora wa mechi, malazi, mashindano na nyinginezo nyingi.
Alisema kuwa kwa sasa ZFF inasaka wadhamini mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo wa sekta binafsi, serikali na watu binafsi.
“Kwa sasa tumekwisha wasilisha barua mbalimbali zilizothibitishwa na serikali kwa ajili ya kusaka wadhamini wa mashindano haya, tunaomba watu binafsi kusaidia mashindano haya,” alisema Vuai.
“Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu shiriki ambazo zipo kwenye maandalizi.”
Alifafanua kuwa mbali ya kusaka wadhamini, pia wanatarajia kufanya tukio la kuchangisha fedha (fund rising gala) kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya mashindano hayo.
“Dhamira yetu ni kufanya mashindano yaliyo bora kabisa na washindi kuzawadiwa zawadi nono za fedha,” alisema.
Alifafanua kuwa wanatarajia kuboresha zawadi za washindi na mikakati yao ni kwa mshindi kukabidhiwa fedha kati ya Sh150 milioni hadi Sh200 milioni .
Aliongeza kuwa katika hafla hiyo mashirika na wadau wataalikwa.
“Tarehe rasmi itatangazwa baada ya kikao chetu na kampuni ya Tanzania Securities Limited kwa kushirikiana na Citadel Tanzania Limited ili kupanga rasmi tarehe na mahali ambapo hafla hiyo itafanyika,” alisema.
Pamoja na kutoweka wazi, gazeti hili limebaini kuwa moja ya bidhaa ambayo itafanyiwa mnada siku hiyo ni jezi iliyosainiwa na Rais wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati kampuni ya Citadel Tanzania Limited na Tanzania Securities Limited zilipomtembelea Ikulu ya Zanzibar.