Dar es Salaam. Sekta ya usanifu na ubunifu wa bidhaa za mapambo nchini imeendelea kukua kwa kasi, ikiibua fursa mpya za ajira kwa vijana na kukuza matumizi ya rasilimali za ndani.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ubora Design, Lucy Kamili, wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya la kampuni hiyo lililopo Slip Way, Masaki jijini Dar es Salaam, Aprili 1, 2026.

Kamili amesema kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh60 milioni kufungua ofisi hiyo, likiwa na lengo la kusogeza karibu huduma na bidhaa zake kwa wateja wa Dar es Salaam na maeneo jirani.

Amesema Ubora Design inajikita katika kubuni na kutengeneza bidhaa za mapambo kwa kutumia malighafi za asili za Kitanzania, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kukuza utamaduni wa nchi.

“Sisi ni Watanzania na tuna uwezo wa kufanya vitu vikubwa. Tunatengeneza bidhaa kwa kutumia malighafi za kwetu kwa sababu bado kuna mtazamo kwamba bidhaa bora zinatoka nje, jambo ambalo si sahihi,” amesema Kamili.

Mmiliki wa ofisi za Ufanisi na usanifu majengo wa Ubora Design, Christopher Lee Plummer(katikati) akikata keki pamoja na wafanyakazi wake, wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo, lililopo Slipway Masaki Jijini Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa kufunguliwa kwaofisi hiyo kutawawezesha wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kupata bidhaa hizo kwa urahisi, badala ya kusafirisha kutoka Arusha kama ilivyokuwa awali.

Kamili amesema tayari kampuni hiyo imeajiri zaidi ya vijana 30 katika shughuli za usanifu na ubunifu, huku ikiendelea kutoa mafunzo kwa wengine ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri.

Kwa upande wake, msanifu majengo ya ndani, Joseph Charles, amewataka vijana kutumia rasilimali za ndani katika ubunifu wao ili kuongeza thamani ya kazi zao na kujitofautisha sokoni.

Amesema mpangilio mzuri wa ndani ya nyumba unaotokana na usanifu bora huongeza thamani na mvuto wa jengo hata kama limejengwa kwa gharama nafuu.

“Tunahitaji pia kuona majengo ya Serikali yakitumia ubunifu wa ndani ili kuonyesha utambulisho wa Kitanzania, kulinda urithi wa taifa na kuvutia wageni,” amesema Charles.

Naye msanifu majengo, Anna Manase, alisema kazi zinazofanywa na Ubora Design zinasaidia kurejesha na kuhifadhi tamaduni za Kitanzania ambazo kwa kiasi kikubwa zilianza kupotea kutokana na kuiga mitindo ya kigeni.

“Ubunifu wetu unalenga kukumbusha jamii umuhimu wa tamaduni zetu katika usanifu na mapambo,” amesema Manase.

Amewashauri vijana wabunifu kuto kata tamaa, bali kuendelea kubuni kazi za kipekee zitakazowatofautisha na wengine sokoni.

Ubora Design yenye makao makuu Arusha ni miongoni mwa kampuni zinazochochea matumizi ya ubunifu wa ndani, kwa kuunganisha ufundi wa asili na mahitaji ya kisasa ya soko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *