Dar es Salaam. Hatua ya uteuzi wa Angela Kizigha kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akiwa bado ni mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), imeibua mjadala, huku wananchi na wachambuzi mbalimbali wakieleza mgongano unaotakana na matakwa ya kisheria.

Wadau wa masuala ya siasa na sheria wamegawanyika kuhusu iwapo hatua hiyo inaendana na sheria za ndani pamoja na masharti ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mjadala huo umechochewa na tafsiri kinzani za kisheria, ambapo wadau wamekuwa na maoni tofauti wengine wakihoji iwapo uteuzi huo una uhalali wa kisheria na kama Kizigha ana nafasi ya kutumikia nafasi zote mbili kwa wakati mmoja.

Alhamisi Aprili 2, 2026, katika teuzi na mabadiliko ya nafasi kwa baadhi ya viongozi wa Serikali, Rais Samia Suluhu Hassan, alimteua Kizigha kuwa ambunge wa Bunge la Tanzania, akitumia mamlaka aliyopewa kisheria kuteua wabunge wa Bunge hilo.

Kufuatia uteuzi wa Kizigha, mjadala katika jamii umekuwa mpana wadau wakihoji ujalali wa uteuzi huo kutokana na Mbunge huyo mteule kuwa Mbunge tayari katika Bunge la EALA akiiwakilisha Tanzania.

Wengine pia wamekuwa wakihoji mgongano wa kanuni za uwakilishi kwa Bunge la EALA na kama zinamruhusu mbunge kuhudumu katika mabunge yote kwa wakati mmoja.

Sheria za ndani

Akifafanua msingi wa kisheria wa uteuzi huo, Wakili Peter Madeleka anasema Rais (Samia Suluhu Hassan) ametumia mamlaka yake halali kikatiba na kwamba hakuna kifungu kinachozuia uteuzi wa mtu anayehudumu EALA kwa sheria za Tanzania.

“Ni sawa kabisa, katika mamlaka ya Rais ya kuteua wabunge, hakuna sehemu amekatazwa asiteue mbunge anayetumikia Bunge la Afrika Mashariki,” amesema Madeleka.

Kwa msingi huo, uteuzi wa Kizigha haukiuki sheria za ndani ya nchi, jambo linaloashiria kuwa hoja ya msingi siyo uhalali wa uteuzi wenyewe, bali ni athari zake katika nafasi nyingine anayoshikilia.

Sheria za Afrika Mashariki na Kanuni za EALA

Hata hivyo, wachambuzi wa sheria za kikanda wanaelekeza mjadala kwenye Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao unaweka mipaka ya wazi kwa wabunge wa Bunge la (EALA) kushika nafasi nyingine za kisiasa au kiutendaji katika nchi zao.

Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe anasema kifungu cha 48 cha mkataba wa EAC kinaweka zuio kwa Mbunge wa EALA kuhudumu katika Bunge, Wizara au utumishi wa Mamlaka ya kiserikali katika nchi yake wakati wa utumishi wake EALA.

“Kifungu cha 48 (6) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kimetamka wazi. Mjumbe wa EALA hatakuwa waziri wa nchi mwanachama au mbunge wa bunge la taifa au mjumbe wa mamlaka ya serikali za mitaa,” amesema.

Kwa tafsiri hiyo, hatua ya uteuzi haizuiwi kufanywa, lakini utekelezaji wake unaathiri moja kwa moja uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi ya ubunge EALA, hatua inayoibua mjadala wa hatua zinazopaswa kufuatwa baada ya uteuzi huu na nafasi ya uwakilishi wa EALA.

Akichambua zaidi kuhusu namna uteuzi wa Kizigha unavyoathiri nafasi yake EALA, Mbunge wa EALA kutokea Tanzania, Wakili Mashaka Ngole anarejea ibara ya 51 ya mkataba huo akisema inaeleza wazi kuhusu uteuzi au uchaguzi wa mbunge wa EALA na mambo yanayomfanya apoteze sifa za kutumikia baraza hilo la wawakishi wa nchi wanachama wa EAC.

“Ukisoma mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ibara ya 51 imeweka masharti kuwa endapo mbunge wa EALA akiteuliwa au kuchaguliwa kuwa mbunge wa bunge la nchi yake anapoteza ubunge wa EALA,” amesema Ngole.

Ameongeza kuwa hali hiyo siyo ya kipekee kwa Kizigha, akitolea mfano wa matukio yaliyotokea awali ambapo wabunge wa EALA walipoteza nafasi zao baada ya kushiriki siasa za ndani ya mataifa yao.

“Hicho kilichotokea kwa Kizigha siyo jambo jipya kwani hata mwaka jana kuna wabunge wawili, Ngwalu Maghembe na James Milya walipoteza nafasi zao EALA baada ya kugombea ubunge hapa nchini.

Hata Uganda kuna mbunge mwenzetu naye amepoteza nafasi yake EALA baada ya kuchaguliwa, hivyo hata kwa huyu itakuwa hivyo,” amesema.

Utaratibu wa kuziba nafasi yake EALA

Akizungumzia hatua inayofuata baada ya uteuzi huu, Ngole amesema Tanzania italazimika kuchagua mbunge mwingine wa EALA baada ya Spika wa EALA kutaarifiwa kuwa nafasi hiyo ipo wazi,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa EALA, Abdullah Makame anaeleza kuwa hatua ya msingi inayobaki ni uamuzi wa mhusika mwenyewe kuhusu kukubali au kukataa uteuzi huo, akibainisha akishakula kiapo cha Ubunge wa Bunge la Tanzania tayari atakuwa amepoteza ubunge wa EALA kwa mujibu wa sheria na kanuni za Bunge hilo.

“Ni heshima kwake kuwa ameteuliwa. Kilichobaki ni yeye kukubali kwa kwenda kula kiapo ambapo atatambuliwa kama mbunge wa Tanzania na kuanzia hapo atakoma kuwa mbunge wa EALA,” amesema Makame.

Amefafanua kuwa baada ya hatua hiyo, taratibu zitakazofuata ni mawasiliano kati ya maspika wa mabunge husika na kuanza kwa mchakato wa kujaza nafasi hiyo kupitia vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni.

Kuhusu Angela Kizigha

Angela Kizigha alichaguliwa kuwa mbunge wa EALA kuwakilisha Tanzania katika muhula wa sasa ulioanza mwaka 2022 ukitarajiwa kukoma ifikapo 2027.

Kizigha ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye amejijengea uzoefu wa kisiasa na kupata ushawishi katika siasa nchini Tanzania na sasa Afrika Mashariki ambapo katika kipindi chake, ameshiriki mijadala ya kitaifa na kikanda katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, utawala bora na maendeleo ya kijamii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki, akijijengea uzoefu wa siasa za kimataifa na ushirikiano wa kikanda.

Alizaliwa katika familia yenye historia ya uandishi wa habari, akiwa mtoto wa marehemu Charles Kizigha, mwandishi mstaafu wa magazeti ya Daily News na Sunday News.

Kizigha aliingia kwa mara ya kwanza katika siasa za EALA mwaka 2012, aliposhinda uchaguzi wa wabunge wa Tanzania kwenda katika bunge hilo kwa kura 166, akiongoza miongoni mwa wagombea wanawake.

Alihudumu katika Mkutano wa Tatu wa EALA (2012–2017), kabla ya kurejea tena mwaka 2022 katika Mkutano wa Tano (2022–2027), ambapo pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kikundi cha Tanzania ndani ya EALA. Katika majukumu hayo, amekuwa akisisitiza kulinda maslahi ya Taifa ndani ya ajenda pana ya ushirikiano wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *