Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesikitishwa na uamuzi wa Serikali kukifungia kituo cha Jambo Online TV kwa muda wa siku 90.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema jukwaa linaamini iwapo kuna makosa ya kitaaluma (kama yapo) yaliyofanywa na mwanahabari mmoja, basi hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mhusika binafsi badala ya kuadhibu chombo kizima cha habari.

Tamko hilo la TEF linatolewa ikiwa imepita siku mbili tangu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilipotangaza kuifungia kwa siku 90 Jambo Online TV (kuanzia Aprili 2, 2026) kwa kile ilichoeleza kuwa imekuwa na mfululizo wa ukiukaji wa sheria, kanuni, masharti ya leseni, maadili, misingi na taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, ilieleza sababu ya kufikia hatua hiyo ni kuwa kwa miezi minne mfululizo kuanzia Septemba 2025, Jambo Online TV kupitia akaunti zake za Instagram na chaneli yake ya utangazaji wa maudhui mtandaoni ya YouTube imekiuka taratibu hizo.

Dk Bakari alisema Machi 31, 2026, Jambo Online TV ilichapisha maudhui ambayo hakuwa na uhakika nayo na yasiyo na uthibitisho.

Maudhui hayo, amesema, yaliupotosha umma kuhusu hali ya matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na matokeo yanayotarajiwa kutoka Tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2020 na 2025,” amesema Dk Bakari.

Ilichosema TEF

Akieleza katika taarifa yake, Balile amesema kwa mtazamo wa kitaaluma, kuwajibisha taasisi nzima kwa makosa ya mtu mmoja ni kinyume na misingi ya haki na uwiano katika utoaji wa adhabu, na hatua hiyo si tu inaathiri uhuru wa chombo husika, bali pia inazuia haki ya umma kupata taarifa na kudhoofisha maendeleo ya taaluma ya habari nchini.

“TEF inatoa mfano wa tukio la Novemba 1, 2007 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo kosa la kitaaluma la daktari kumfanyia mgonjwa upasuaji wa mguu badala ya kichwa na mwingine kufanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya goti halikusababisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufungwa, bali wahusika binafsi waliwajibishwa,” amesema Balile.

Kwa msingi huo, amesema TEF inaona hatua ya kufungia Jambo Online TV inaweza kutafsiriwa kama kukiuka misingi ya haki na taaluma.

“TEF inasisitiza kuwa kufungia chombo cha habari ni adhabu inayowaathiri pia wananchi, kwani inawanyima fursa ya kupata taarifa. Hivyo, si suluhisho la kitaaluma linalofaa katika kushughulikia makosa ya mtu mmoja,” amesema Balile.

Kwa kuzingatia hilo, TEF imependekeza kufanyika kwa mazungumzo ya kitaaluma kati ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jambo Online TV na mwandishi husika.

Amesema lengo la mazungumzo hayo ni kupata suluhisho la haraka, lenye kuzingatia haki, kulinda maslahi ya taifa, taaluma ya habari, na hadhira ya ndani na nje ya nchi.

“TEF inahitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuzingatia nidhamu ya kitaaluma kwa uwiano na haki, bila kuwaadhibu wadau wengine wasiohusika,” imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *