Nigeria. Chama cha DJs nchini Nigeria (NDJ) kimepiga marufuku DJ’s wote kupiga nyimbo za mwanamuziki Burna Boy ndani na nje ya nchi.
Chama hicho kimeeleza kuwa marufuku hiyo inawahusu ma-dj wote wanaofanya kazi chini yake bila kujali wapo pande zipi za dunia.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mkali wa Afrobeat Burna kuzichapa na Dj Tunez kwenye tamasha linalofanyika jijini Lagos kila wiki la Obi’s House.
Inaelezwa tukio hilo ambalo limetokea mapema wiki hii lilianza kwa mabishano baina ya Burna na Dj Tunez ambapo baada ya muda ugomvi ulikuwa mkubwa huku vijana na walinzi wa Burna wakichangia kumpiga Dj huyo.
Sababu za ugomvi huo bado hazijajulikana. Lakini baadhi ya mashabiki wanadai, Dj Tunez amekuwa hapendezwi na kitendo cha watu kumfananisha Wizkid na Burna Boy akidai kuwa Kid hatendewi haki kwenye hilo.
Aidha baada ya tukio hilo, chama cha DJ kilitoa taarifa katika ukurasa wao wa Instagram wakiitaka jamii kuacha ubaguzi, chuki pia kuwapa heshima.
“Hakuna mtu anayezaliwa akimchukia mwingine kwa sababu ya rangi, dini, asili au jinsia. Watu hujifunza chuki, na kama wanaweza kujifunza kuchukia, pia wanaweza kufundishwa kupenda, kwa sababu upendo ni wa asili moyoni mwa binadamu.
“DJ wote ni sawa na wanapaswa kuheshimiwa kwani tunatoa msaada wa wazi kusaidia wateja kufanikiwa malengo yao ndani na nje ya nchi. Uhuru na usawa kwa DJ wote ni muhimu ili wote waweze kustawi. Hatuwezi sote kufanikisha ikiwa nusu yetu inashikiliwa nyuma,” imeeleza taarifa hiyo
Aidha imeendelea ikieleza “Muziki wa Burna Boy utaondolewa kwa muda kwenye Playlist za DJ wote hadi pale tutapowapa taarifa kwa sasa timu yetu itafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la usiku wa jana linalomuhusisha Dj Tunez,”imeeleza taarifa hiyo