Nchini Nigeria, mashambulizi ya kijeshi yaliyotekelezwa kimakosa yamesababisha vifo vingi na majeraha mengi, shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International limetangaza siku ya Jumapili, Aprili 13.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo lilitokea siku ya Jumamosi alasiri katika mji wa Jilli, katika Jimbo la Yobe, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Jeshi, likiamini kwamba lilikuwa likiwashughulikia waasi wa Boko Haram, lilianzisha mashambulizi ya angani dhidi ya umati wa watu sokoni, kulingana na vyanzo vingine.

Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi haya ya kijeshi inatofautiana kulingana na vyanzo mbalimbali. Siku ya Jumapili Amnesty International iliripoti kwamba zaidi ya watu 100 waliuawa katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, ikilaani shambulio hilo la angani na kutoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi usioegemea upande wowote.

Kulingana na Issa Sanoussi, mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria, ndege za kijeshi ziliwafyatulia risasi watu katikati ya soko, zikidhani kuwa ni waasi wa Boko Haram. “Kulikuwa na mashambulizi ya anga siku ya Jumamosi usiku, wakati soko likiwa limejaa watu wengi. Hili ni soko linakuwepo kila mwishoni mwa wiki hapa kati ya miji ya Borno na Yobe. Jeshi lilifika na kudondosha mabomu sokoni. Walisema walikuwa wanatafuta waasi, lakini maelezo yao yanaibua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu. Kwa sababu watu wanajiuliza kwa nini kuna raia wengi waliouawa katika matukio ya aina hii wakati jeshi linadai kuwasaka waasi. Mwishowe, ni raia wanaouawa, watu wa kawaida; haikubaliki kabisa.” 

Shirika la haki za binadamu linatoa wito wa uchunguzi ili kubaini sababu na viwango mbalimbali vya uwajibikaji kuhusu kosa hili: “Tunalaani shambulio hili na kutoa wito wa uchunguzi. Tunatoa wito kwa serikali ya Nigeria kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika na mauaji haya wanafikishwa mbele ya haki na kushtakiwa. Uchunguzi sahihi na ulio wazi pekee ndio unaoweza kuthibitisha uwajibikaji. Tunaamini kwamba watu wengi sana wameuawa, wakiwemo watoto. Na hilo ni kinyume cha sheria za kimataifa.”

Lawan Zanna Nur, kiongozi wa eneo hilo, alitaja idadi kubwa zaidi ya vifo ya watu 200 waliouawa na kujeruhiwa. Kulingana na vyanzo kutoka eneo la tukio, ndege tatu za kijeshi, kulingana na mashahidi, zilikuwa zikiwafuatilia wanajihadi wa Boko Haram ambao wanaenea katika eneo lote.

“Soko la Jilli huvutia wafanyabiashara kutoka mbali kama majimbo ya Kano na Jigawa (kaskazini magharibi).” Soko hilo linadhibitiwa kikamilifu na Boko Haram, ambayo inajihusisha na usalama na kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara. “Tumekuwa tukichunguza soko hili kwa muda mrefu,” chanzo ndani ya idara ya ujasusi ya Nigeria kimeliambia shirika la habri la AFP.

Jeshi la Nigeria, lililohusika katika mashambulizi hayo, bado halijatoa maoni yoyote, na wala mamlaka katika mji mkuu wa shirikisho, Abuja. Kama ukumbusho, matukio kama hayo huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, huku uchunguzi ukitangazwa lakini matokeo yake hayajawahi kutolewa hadharani.

Nchini Nigeria, matukio kama hayo huripotiwa mara kwa mara, kama vile mnamo mwezi Juni 2025 wakati raia 20 waliuawa na shambulio la anga katika Jimbo la Zamfara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *