Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, ametoa tamko kufuatia shambulio la Marekani dhidi ya meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Oman, akisema kwamba kuweka mzingiro dhidi ya bandari za Iran ni uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Katika ujumbe kwenye ukurasa wake wa X siku ya Araghchi amesema:

“Kuweka mzingiro katika bandari za Iran ni kitendo cha kivita, na hivyo ni uvunjaji wa wazi wa usitishaji wa mapigano.”

Ameongeza kuwa: “Kushambulia meli ya kibiashara na kuwakamata mabaharia wake ni ukiukaji mkubwa zaidi.”

Alisisitiza pia: “Iran inajua namna ya kuvunja vizuizi, namna ya kutetea maslahi yake, na namna ya kukabiliana na vitisho.”

Mapema Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje katika taarifa yake ililaani vikali shambulio hilo la Marekani dhidi ya meli ya Iran, ikitaja shambulio hilo kuwa “si tu kwamba linakwenda kinyume na misingi ya msingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, bali pia ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji wa mapigano yaliyoanza kutekelezwa Aprili 8, na ni kitendo cha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Wizara hiyo ilitoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO), pamoja na serikali husika kuchukua hatua “thabiti na kali” dhidi ya “kitendo cha uhalifu” dhidi ya usafiri wa kimataifa wa kibiashara.

Aidha, ilitoa onyo kuhusu “athari hatari sana” zinazoweza kujitokeza kutokana na “kitendo cha Marekani kisicho cha halali”, ikisisitiza haja ya kuachiliwa mara moja kwa meli hiyo na wafanyakazi wake.

Wakati huo huo, Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, yaliyo chini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), yametoa onyo kwa Marekani dhidi ya kukamata meli za kibiashara za Iran katika Bahari ya Oman. Taarifa hiyo imesemaVikosi vya Ulinzi vya Iran vitachukua hatua dhidi uharamia unaofanywa na jeshi la Marekani.

Taarifa hiyo pia imelaani hatua ya Marekani ya kuvunja zaidi usitishaji wa mapigano na kujihusisha na “uharamia wa baharini”, baada ya kufyatua risasi kuelekea moja ya meli za kibiashara za Iran katika Bahari ya Oman.

Wakati huo huo, Jeshi la Wanamaji la IRGC limetangaza kuwa, meli mbili zinazohusishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, ambazo zilikuwa zikijaribu kuondoka kwa siri kupitia Lango Bahari Hormuz bila kibali na huku zikifanya makosa ya mara kwa mara, zilitambuliwa na kusitishwa safari zao. Meli hizo zimeelekezwa katika bandari za Iran kwa uchunguzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *