
Amir Saeed Iravani, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, ametoa malalamiko makali kuhusu matumizi mabaya ya Marekani ya ardhi na anga ya nchi tano za eneo katika hujuma za kijeshi dhidi ya Iran. Nchi hizo ambazo zimeafiki ardhi zao kutumiwa kuishambulia Iran ni pamoja na Qatar, Kuwait, Bahrain, Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia.
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatano, katika barua zake tofauti kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kwa Baraza la Usalama, alisema:
“Kwa kuzingatia uwajibikaji wa kimataifa wa serikali zinazotoa ardhi au anga yao kutumiwa na wengine kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya uchokozi na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya ardhi ya nchi ya tatu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatangaza kwa uwazi na kwa ukali malalamiko yake dhidi ya hatua hizo zinazokiuka sheria za kimataifa.”
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa:
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uwazi inazitaka serikali za Qatar, Kuwait, Bahrain, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia zizingatie misingi ya ujirani mwema, na zikomeshe kuendelea kuruhusu ardhi na anga yao kutumiwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Katika barua hizo kuna nyaraka zenye ushahidi kamili kuhusu namna nchi hizo zilivyotumiwa na maadui kutekeleza hujuma dhidi ya Iran.
Ikumbukwe kuwa katika kujibu hatua hizo wakati wa vita vya siku 40, Iran ilitekeleza mashambulizi yakulipiza kisasi katika kambi za kijeshi na ngome za kiuchumi na kiusalama za Marekani na utawala haramu wa Israel katika nchi hizo za Kiarabu.
Wakati huohuo na sambamba na kuchapishwa kwa barua hii, kamanda wa majeshi ya kigaidi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi amekuru kuwa Bahrain, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Qatar, Kuwait na Jordan zilitoa ushirikiano wa kiwango cha juu sana katika vita dhidi ya Iran.
Brad Cooper aliongeza kuwa nchi hizo, kwa kuweka ardhi na vituo vyao vya kijeshi katika matumizi ya Marekani, zimesaidia katika mashambulizi ya anga, makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya miji mbalimbali ya Iran.