Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Benki ya Azania PLC, zimekubaliana kufanikisha matibabu ya watoto 250 wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Aprili 23, 2026 Jijini Dar es Salaam, yakilenga kugharamia matibabu ya watoto 250 kupitia mbio fupi za MOI Marathon zinakazotimua vumbi Oktoba 25, mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya amesema ushirikiano huo utaiwezesha Azania Benki kutoa kiasi cha Sh200 milioni kwa mwaka kugharamia matibabu ya watoto hao.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam baada ya makubaliano  na Benki ya Azania kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

“Azania Benki imekuja wakati muafaka wakati tunaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa MOI ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika na kuhitimishwa na mbio fupi za MOI marathon” amesema Dk Mpoki na kuongeza kuwa,

“Makubaliano haya yatadumu kwa miaka mitatu na yatawezesha matibabu ya watoto wetu wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi, ambao kila vizazi hai 1000 watoto saba huzaliwa na tatizo hilo,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Azania Bank, Yahaya Mbanka amesema benki hiyo inajivunia kurudisha sehemu ya faida yake kwa kusaidia matibabu ya watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi kupitia MOI Marathon.

“Katika makubaliano haya Azania Benki inakwenda kutoka Sh 200 Milioni kwa taasisi ya MOI kupitia MOI marathon ili kuunga mkono jitihada za MOI kutoa matibabu kwa watoto hawa,” amesema.

Sababu ya matatizo hayo

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya afya, tatizo la kujifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi linaepukika.

Mkurugenzi  Mtendaji wa MOI Dk Mpoki Ulisubisya (kulia) akionyesha mkataba wa makubaliano na Mkurugenzi  wa Maendeleo ya Biashara Azania Bank, Yahaya Mbanka kwa ajili ya kuhudumia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Kinachotakiwa kwa kina mama wajawazito ni kupewa uelewa wa kutosha kuhusu lishe hasa katika kipindi cha ujauzito.

Hata hivyo, inaonekana kunahitajika kazi ya ziada kwa sababu uelewa miongoni mwa kina mama bado ni mdogo.

Sababu kuu ya tatizo hilo ni utapiamlo kwa akina mama kabla ya kupata ujauzito. Utapiamlo huo ni ukosefu wa madini ya folic acid unaotokana na kutokula vyakula vinavyotakiwa.

Akina mama wanashauriwa  kabla ya kubeba mimba wahudhurie kliniki  wapate ushauri kwa wataalmu afya, kuna vyakula kama mbogamboga, matunda, vyakula vyenye nyuzi nyuzi, maziwa na pia kuna vidonge.

Kulingana na takwimu za mwaka jana za MOI, katika kila vizazi 1,000 watoto watatu wanzaliwa na tatizo hilo huku kwa kila mwaka wakizaliwa watoto 4,800.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *