Kutoka Johannesburg, balozi wa Ufaransa nchini Afrika Kusini, David Martinon, ametumia fursa ya mkutano na waandishi wa habari kkubainisha nia ya Ufaransa ya kuona Pretoria ikirejeshwa kwenye mikutano ya G20, baada ya nchi mwenyeji, Marekani, kuiondoa kiholela katikati ya mvutano mkubwa wa kidiplomasia. Kwa hivyo, wawakilishi wa Afrika Kusini hawakuweza kushiriki katika mikutano ya kwanza ya G20 ambayo tayari imefanyika.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu huko Johannesburg, Valentin Hugues

Donald Trump alipotangaza kuiondoa Afrika Kusini kiholela kutoka G20 mwezi Novemba mwaka uliyopita, Ujerumani ilijibu mara moja, ikisema kwamba itafanya kila linalowezekana kumshawishi rais wa Marekani abadilishe mawazo yake. Hivi majuzi, Brazil pia imekuja juu na kuitetea Pretoria.

Na kulingana na Balozi David Martinon, Ufaransa pia inajaribu kutatua hali hiyo. “Suala hili limeibuliwa mara kadhaa na washauri wetu wa kidiplomasia,” alielezea balozi wa Ufaransa. “Ni wazi tunaiona Afrika Kusini kama mwanachama wa G20 na kuwa na wajibu wa kushiriki katika mikutano yake yote.”

Hasa kwa kuwa Afrika Kusini ni mwanachama wa kudumu na mwanzilishi wa kundi la 20, na kwa kawaida, nchi haiwezi kuamua kujiondoa yenyewe. Kama ukumbusho, Donald Trump alisusia mkutano wa G20 huko Johannesburg mwaka jana, wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulikuwa katika kiwango cha chini kabisa.

Wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari huko Johannesburg, David Martinon pia alirejelea mkutano wa kilele wa G7 nchini Ufaransa na mwaliko uliotolewa kwa Kenya, badala ya Afrika Kusini, ingawa Pretoria hapo awali ilidai kuwa kwenye orodha ya wageni. Alidai kwamba ni nchi nne pekee zilizoalikwa. “Na tulichagua Kenya kwa sababu tunaona mkutano wa kilele wa Africa Forward kuwa, kwa njia fulani, sehemu muhimu ya urais wa G7 wa Ufaransa,” mwanadiplomasia huyo alielezea.

Mkutano wa kilele wa Africa Forward, unaoandaliwa kwa pamoja na Ufaransa na Kenya, utaanza mnamo Mei 11 katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *