
Wakati mawingu mazito yanapotanda na matone ya kwanza ya mvua yanapoigusa ardhi kavu, kuna harufu fulani ya kipekee, ya udongo na ya kuburudisha inayotanda hewani.
Kwa wengi, harufu hii huleta kumbukumbu za utotoni, amani, na utulivu wa ghafla. Lakini je, unajua kuwa harufu hiyo si burudani tu kwa pua, bali ni tiba ya kisaikolojia iliyothibitishwa kisayansi kupambana na msongo wa mawazo na sonona?
Wataalamu wa sayansi ya ubongo na saikolojia sasa wanabainisha kuwa harufu hii, inayojulikana kitaalamu kama Petrichor, ina uwezo wa kurekebisha mfumo wa neva na kuleta utulivu wa akili ndani ya sekunde chache.
Neno “Petrichor” lilibuniwa mwaka 1964 na watafiti wa Australia, Isabel Joy Bear na Richard Thomas. Linatokana na maneno ya Kigiriki “petra” (jiwe) na “ichor” (majimaji yanayotiririka kwenye mishipa ya miungu).
Harufu hii inasababishwa na mchanganyiko wa mafuta asilia kutoka kwenye mimea na kemikali ya Geosmin, inayozalishwa na bakteria wa udongo (actinomycetes).
Mvua inaponyesha, matone yanatengeneza viputo vidogo vya hewa (aerosols) ambavyo husambaza Geosmin hewani.
Pua ya binadamu ina uwezo wa ajabu wa kutambua Geosmin hata ikiwa katika kiasi kidogo sana. Geosmin ndio inayosababisha harufu baada ya mvua kunyesha.
Harufu hii inavyotibu akili
Mfumo wetu wa kunusa umeunganishwa moja kwa moja na Amygdala na Hippocampus, yaani sehemu za ubongo zinazohusika na hisia na kumbukumbu.
Tofauti na milango mingine ya fahamu, harufu haiendi kwanza kwenye “kituo cha kulelea habari” bali hugusa hisia moja kwa moja.
Dk Diana Bolden, mtaalamu wa tiba asilia ya harufu, anafafanua:”Mvua inaponyesha na harufu ya udongo kutanda, ubongo hutoa kemikali za ‘furaha’ kama serotonini na dopamini. Hii inapunguza kiwango cha homoni ya cortisol, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha msongo wa mawazo na wasiwasi.”Wataalamu wa afya ya akili wameanza kupendekeza tiba ya asili kama sehemu ya matibabu ya kisasa.
Dk Andrew Weil, bingwa wa tiba mseto na mwandishi maarufu wa vitabu vya afya, anasema katika moja ya maandiko yake: “Binadamu ana uhusiano wa kibaolojia na mvua. Kwa mababu zetu, harufu ya mvua ilimaanisha uhai, chakula, na usalama. Hadi leo, harufu hiyo inapotufikia, mfumo wetu wa neva unajihisi kuwa katika ‘usalama’, hali inayozima mfumo wa ‘pambana au kimbia’ (fight or flight) unaosababisha msongo.”
Pia, mwanabiolojia mashuhuri Edward Wilson, kupitia nadharia yake ya ‘Biophilia’, anaeleza kuwa binadamu ana upendo wa asili kuelekea viumbe hai na mifumo ya asili. Harufu ya mvua ni kiunganishi cha msingi kati ya binadamu na ulimwengu wake wa asili.
Faida tano za harufu ya mvua
Mosi, kupunguza wasiwasi: Harufu ya Geosmin ina athari ya kutuliza ambayo hupunguza mapigo ya moyo yaliyoenda mbio kutokana na hofu.
Pili, kuboresha usingizi: Mazingira ya mvua na harufu yake huandaa ubongo kulala, ndiyo maana watu wengi hupata usingizi mzito mvua ikinyesha.
Tatu, kusafisha mawazo: Hewa ya baada ya mvua huwa na ioni hasi (negative ions) nyingi. Ioni hizi zikifika kwenye mfumo wa damu, huongeza ufanisi wa oksijeni kufika kwenye ubongo, jambo linaloongeza umakini na utulivu.
Nne, kurejesha kumbukumbu chanya: Kwa watu wengi, mvua huwakumbusha nyakati tulivu, hivyo kuusaidia ubongo kuhama kutoka kwenye mawazo mabaya ya sasa kwenda kwenye kumbukumbu tulivu.
Tano, tiba ya unyogovu. Kutoka nje na kuvuta hewa safi ya mvua husaidia kuvunja mzunguko wa mawazo ya kujirudia ambayo ni sifa kuu ya unyogovu.
Katika zama hizi za kelele za miji, teknolojia, na shinikizo la maisha, msongo wa mawazo umekuwa janga lisiloonekana.
Tunapotafuta tiba kwenye vidonge na vinywaji, tusisahau kuwa suluhu nyingine ipo angani na ardhini.
Harufu ya mvua si tu tukio la kikemia; ni wimbo wa asili unaoipoza roho. Wakati mwingine mvua itakaponyesha, usilaumu tope au baridi—simama, vuta pumzi, na ruhusu “Petrichor” itibu akili yako.
Kama asili inavyojifanya upya kupitia maji, nawe unaweza kujifanya mpya kupitia harufu yake.
Makala hii inatokana na vyanzo mbalimbali vya kimtandao