Dar es Salaam. Mara nyingi uhusiano wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Harmonize na Kajala Masanja umekuwa ukigonga vichwa vya habari hasa mtandaoni kutokana na jinsi wanavyosimamia mambo yao mbele ya umma.
Kajala, staa wa filamu kwa miaka mingi, yeye na Harmonize ni kama wamechagua dunia yao huku wakipitia pamoja pande shuka za uhusiano wao kwa zaidi ya miaka mitano sasa tangu walipojitokeza pamoja hadharani.
Hata hivyo, licha ya yote yaliyotokea na yanayoendelea kuzungumzwa kati yao, Kajala anaendelea kuacha alama katika maisha binafsi ya Harmonize na kwa upande wa chapa yake kimuziki na kibiashara akiweka rekodi hizi tano zifuatazo.
1. Pete mara mbili
Kajala ndiye mwanamke pekee ambaye Harmonize amemvisha pete ya uchumba mara mbili – tukio la kwanza lilifanyika Juni 25, 2022 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, ikiwa ni kipindi kifupi baada ya wao kurudiana.
Tukio la pili lilikuwa Desemba 29, 2025, ndani ya boti (yacht) katika Bahari ya Hindi na mastaa kadhaa walipata mwaliko akiwemo binti wa Kajala, Paula.
Ikumbukwe tukio hilo la mwisho lilikuja wiki kadhaa baada ya kuwepo tetesi za wao kurudiana, na siku moja baada ya Kajala kupandishwa jukwaani na Harmonize katika shoo yake iliyofanyika Zanzibar.
Kwa jumla Kajala anakuwa mrembo wa pili kuvishwa pete na Harmonize baada ya aliyekuwa mke wa mwanamuziki huyo, Sarah ambaye ndoa yao ilidumu kwa takribani mwaka mmoja huku uhusiano ukichukua miaka zaidi ya mitatu.
2. Kawa meneja wake
Kuna kipindi Harmonize alimtangaza Kajala kuwa meneja wake pamoja na kusimamia baadhi ya shughuli za Konde Music Worldwide, hatua ambayo iliibua minong’ono kwa baadhi ya mashabiki kwa sababu mrembo huyo inaonyesha hana uzoefu huo.
Wengine walienda mbali zaidi na kudai Harmonize amemuiga mwimbaji wa Nigeria, Wizkid ambaye mpenzi wake Jada P ndiye meneja wake na amempatia mafanikio makubwa ikiwemo kushinda Grammy.
Ingawa kwa sasa Kajala hayupo tena katika nafasi hiyo, bado anasalia kuwa mwanamke pekee aliyewahi kuwa na uhusiano na Harmonize ambaye alipata nafasi ya kuwa meneja wa mwanamuziki huyo ingawa alihudumu kwa muda mfupi sana.
3. Video tatu pamoja
Hadi sasa Kajala ameonekana katika video tatu za nyimbo za Harmonize wakiigiza pamoja kama wapenzi waliopendana na kushibana, hatua inayomfanya bibie kuwa mrembo pekee aliyefanya video nyingi zaidi za mwimbaji huyo.
Kajala ameonekana katika video za nyimbo kama Nitaubeba (2022), Wewe (2026) na Kama Sio (2026) ambao Harmonize ameshirikiana na Kusah, video hii ya mwisho imefanya mwanamuziki huyo kukosolewa sana mitandaoni.
Hoja za wakosoaji ni Harmonize anafanya muziki kwa ajili ya mashabiki wake na si Kajala hivyo aache kumtumia katika video zake kila wakati, na hata kumwambia yeye tu kitu kinachofanya muziki wake kuwa kawaida.
Hata hivyo, Harmonize ameonyesha kupuuzia ukosoaji huo akisema yeye ndio huwa anamlazimisha Kajala kufanya naye kazi na ni kwa sababu maalum. Mfano video hii ya mwisho kutoa, anasema hakuona mrembo anayeweza kuvaa uhusika wa umalkia na ndipo akamtumia Kajala.
4. Amtungia nyimbo kibao
Kuna nyimbo zaidi ya sita ambazo Harmonize amemwimbia Kajala au amezitoa kutokana na matukio yaliyoukumba uhusiano wao ambao unatajwa kuwepo miaka kabla ya kuanza kuonekana hadharani mapema 2021.
Hata hivyo, kuna nyimbo tatu ambazo jina la Kajala limetajwa moja kwa moja, nyimbo hizo ni Zilipendwa (2017), Mtaje (2021) na Deka (2022), hakuna mrembo mwingine amewahi kupata bahati kama hii kutoka kwa Harmonize.
Hivyo katika panda shuka zake na Kajala, Harmonize ametumia sana muziki wake kuweka mambo sawa baina yao na hata kueleza hisia zake pale alipoumizwa au kufurahishwa na mwenzake kwa lolote lile.
5. Magari ya kifahari
Katika wimbo wake, Deka (2022) akilishirikisha kundi la Mabantu, Harmonize anadai amemnunulia Kajala magari mawili aina Range Rover, huku rekodi zikionyesha hiyo ni mara ya kwanza kwake kufanya hivyo kwa mpenzi wake.
“Kajala one and two tena zote ni range. Mwenzetu umetuma ka laki tu na bado unauliza chenji,” anaimba Harmonize katika wimbo huo uliotayarishwa na Sign Beat.
Hata hivyo, kufikia Desemba 2022, wawili hao waliachana kwa mara nyingine tena huku kukiwa na madai Kajala alichukua gari alilozawadiwa na kwenda kulificha akihofia kupokonywa baada ya penzi kufa.
Harmonize ambaye sasa yupo na Kajala, hivi karibuni alidai magari anayomiliki yana thamani ya Sh2 bilioni, akiyataja magari yao ni V8 mbili, Range Rover Sport, Range Rover Defender, na BMW 4 Series, hivyo kumpa mpenzi wake gari si suala kubwa.