
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Tanzania, kwa kushirikiana na Foundation for Civil Society (FCS), limezindua mpango wa kuimarisha uwezo wa asasi za kiraia (AZAKi) zinazoongozwa na vijana na wanawake katika mikoa ya Dar es Salaam, Songwe na visiwa vya Zanzibar.
Mpango huu ni hatua muhimu kwa FCS kuingia katika ushirikiano wake wa kwanza wa moja kwa moja na Umoja wa Mataifa, jambo linaloonesha maendeleo katika jitihada za kuendeleza suluhisho za ndani kwa ajili ya watoto na vijana walio katika mazingira hatarishi nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Ijumaa Aprili 24, 2026, Mkuu wa Ulinzi wa Mtoto wa UNICEF Tanzania, Miranda Armstrong, alisema mpango huo umebuniwa kuwa na athari ya muda mrefu.
“Kwa kuwekeza katika uwezo wa muda mrefu wa AZAKi zinazoongozwa na vijana na wanawake, mpango huu unazipa nguvu za kitaasisi na kiutendaji zitakazozisaidia kuendelea hata baada ya ufadhili wa miradi kumalizika,” alisema.
Alibainisha kuwa zaidi ya asasi 30 zitanufaika na mafunzo ya vitendo kuhusu uandaaji wa miradi na namna ya kushughulikia masuala ya ulinzi wa mtoto, huku asasi 15 zikitarajiwa kupata ruzuku ya Sh25 milioni kila moja baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.
Armstrong alisema juhudi hizo zitalenga kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake, kupunguza mimba za utotoni na kuboresha afya ya uzazi kwa vijana.
Aliongeza kuwa mpango huo unakuja katika wakati muhimu ambapo ufadhili wa maendeleo duniani, hususan katika masuala ya usawa wa kijinsia na ulinzi wa mtoto, unaendelea kupungua.
“Huu ni wakati muhimu wa kuimarisha majibu ya ndani. Hata hatua ndogo zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wavulana na wasichana,” alisema.
Uteuzi wa maeneo ya kipaumbele ulizingatia takwimu, ambapo Songwe imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha mimba za utotoni nchini, huku ongezeko la kasi la watu katika Jiji la Dar es Salaam likileta changamoto za kipekee kwa mipango inayolenga vijana. Mpango huo pia utaenea katika mikoa mingine ikiwemo Kigoma na Tabora.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Dar es Salaam, Given Sure, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wakati wa uzinduzi huo.
“Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika safari yetu ya kujifunza, na tunajivunia kutembea pamoja na washirika wetu wa AZAKi huku tukikua, kujifunza na kuleta mabadiliko ya kudumu,” alisema.
Alisema kuimarisha AZAKi zinazoongozwa na vijana na wanawake kunalingana na vipaumbele vya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, ambao unasisitiza maendeleo jumuishi na majibu yanayoongozwa na jamii.
Idadi kubwa ya vijana nchini Tanzania ni fursa lakini pia ni changamoto ya haraka, ambapo vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 19 wanachukua takribani asilimia 23 ya idadi ya watu. Hata hivyo, wengi wao wanakumbana na changamoto kama mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ukatili, upatikanaji mdogo wa huduma rafiki kwa vijana, na ushiriki mdogo katika maamuzi.
Maofisa wanasema AZAKi zinazoongozwa na vijana na wanawake ziko katika nafasi nzuri ya kushughulikia changamoto hizi kutokana na ukaribu wao na jamii, hali inayowawezesha kujibu kwa haraka, kujenga imani na kuhamasisha mabadiliko.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mkuu wa Programu Ubora na Mafunzo kutoka FCS, Cynthia Bavo, alisema mradi huo unalenga kuimarisha asasi zinazofanya kazi na vijana na wanawake.
“Tumezindua mradi unaolenga kuwawezesha asasi za kiraia zinazoongozwa na vijana na wanawake, pamoja na zile zinazotekeleza programu zinazolenga makundi haya,” alisema.
Mpango huo unaoungwa mkono na UNICEF na kutekelezwa na FCS utatoa mafunzo kwa AZAKi 30, huku 15 zikichaguliwa kupata ufadhili baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.