Wataalamu wa malezi na makuzi ya watoto mkoani Tanga wameeleza wasiwasi wao kuhusu shinikizo linaloongezeka kwa watoto, wakisema wengi wananyimwa haki yao ya msingi ya kucheza, kupumzika na kukua katika mazingira salama na yenye afya.

Wanasema hali hiyo inaweza kuathiri maendeleo ya kimwili na kiakili ya watoto ikiwa hatua hazitachukuliwa mapema.

Wasiwasi huo ulielezwa wakati wa warsha ya siku mbili kuhusu malezi, ukuaji na maendeleo ya mtoto katika umri wa awali, iliyohudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akizungumza katika warsha hiyo hivi karibuni, mtaalamu wa maendeleo ya mtoto, Bruno Ghumpi, alisema ukuaji wa mtoto huanza kuzingatiwa tangu akiwa tumboni mwa mama yake.

Alisema mama mjamzito anapaswa kupata lishe bora, huduma za afya pamoja na ulinzi na usalama, kwa kuwa afya ya mtoto hutegemea afya ya mama tangu kipindi cha ujauzito.

“Ili mtoto akue katika utimilifu wake, mama mjamzito anapaswa kupata lishe bora na huduma za afya. Baada ya kuzaliwa pia mtoto anahitaji ulinzi, usalama pamoja na fursa ya kujifunza kupitia malezi yenye mwitikio kutoka kwa wazazi na walezi,” alisema.

Aliongeza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya ukuaji wa mtoto, kwani kupitia kucheza mtoto,  hujifunza mambo mbalimbali na kukuza uwezo wake wa kufikiri.

“Watoto wanahitaji kucheza kwa sababu kucheza kwa mtoto ni kama kazi yake. Kupitia michezo mtoto hujifunza mambo mengi na ubongo wake hukua vizuri. Wazazi wanapaswa kuwapa watoto muda wa kucheza ili kuwasaidia kukuza uwezo wao wa kufikiri,” alisisitiza.

Ghumpi alibainisha kuwa lishe bora pia ina mchango mkubwa katika maendeleo ya ubongo wa mtoto. Alisema mtoto asipopata lishe sahihi anaweza kuwa na maendeleo hafifu ya kiakili.

Alitaja mambo nane muhimu yanayochangia ukuaji mzuri wa ubongo wa mtoto kuwa ni lishe bora, michezo, kupumzika, upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa, afya bora, ulinzi na usalama wa mtoto, uchangamshwaji wa awali pamoja na upatikanaji wa vifaa vya michezo.

“Vitu hivi ndivyo vinavyojenga msingi wa ukuaji wa ubongo wa mtoto. Mtoto akipata mazingira haya tangu utotoni ana nafasi kubwa ya kukua akiwa na uwezo mzuri wa kufikiri na kujifunza,” alisema.

Aidha, alionya kuwa watoto wengi, hasa katika baadhi ya shule binafsi, wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa masomo unaowanyima muda wa kucheza na kupumzika.

“Watoto wanatumia muda mwingi darasani na wanaporudi nyumbani wanapewa kazi nyingi za nyumbani, hata wakati wa likizo. Bila kucheza na kupumzika tunawanyima nafasi ya kukua na kuwa watu wazima wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa lishe wa Mkoa wa Tanga, Sakina Mustapha, alisema lishe timilifu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya mtoto tangu akiwa tumboni.

Alisema mtoto asipopata lishe bora anaweza kuzaliwa akiwa na uzito pungufu au hata kupoteza maisha.

“Programu hii inalenga watoto kuanzia umri wa sifuri hadi miaka nane. Hivyo tunaanza kumuangalia mtoto akiwa tumboni mwa mama yake kwa kuhakikisha mama anahudhuria kliniki na anapata vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto,” alisema.

Aliongeza kuwa mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo kabla ya kuanza kupewa vyakula vya ziada.

“Tunasema mtoto anyonye maziwa ya mama pekee hadi miezi sita. Baada ya hapo anaweza kuanza kupewa vyakula mchanganyiko kwa sababu maziwa ya mama pekee hayawezi kukidhi mahitaji yote ya lishe,” alisema.

Sakina alisema mtoto anapaswa kuendelea kupata lishe bora hadi kufikisha angalau miezi 24 huku akiendelea kupitia hatua mbalimbali za ukuaji.

Aliongeza kuwa baada ya miaka miwili mtoto anaweza kuanza elimu ya awali huku akiendelea kula vyakula mchanganyiko vinavyosaidia maendeleo yake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya United Help for Tanzania Children (UHTC), Regis Temba, alisema taasisi hiyo imepanga kuanzisha maeneo maalum ya kucheza katika vituo vitano vya afya ndani ya Jiji la Tanga.

Alisema lengo ni kubadilisha mazingira ya kliniki ili yawe rafiki zaidi kwa watoto na wazazi wanaofika kupata huduma.

“Tunataka watoto wanapokuja kliniki wasione ni sehemu ya sindano na matibabu pekee, bali waweze pia kucheza na kujifunza kupitia michezo mbalimbali inayochochea ukuaji wa ubongo,” alisema.

Alitoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya afya kuandaa mazingira yatakayowezesha kuanzishwa kwa maeneo hayo ili kuwapa watoto nafasi ya kucheza na kujifunza tangu wakiwa wadogo.

Kwa ujumla, washiriki wa warsha hiyo walisisitiza kuwa maendeleo ya mtoto hayapaswi kupimwa kwa ufaulu wa masomo pekee, bali yanahitaji pia lishe bora, ulinzi, malezi sahihi na muda wa kucheza ili kujenga kizazi chenye afya, maarifa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *