
BAADA ya Simba kutangaza uwanja wake wa nyumbani kwenye mechi ya Kariakoo Dabi, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Rodgers Gumbo, amesema wako tayari kukutana na Wekundu hao kwani wanaujua vyema uwanja ambao watakwenda kucheza.
Hapo awali maswali yalikuwa mengi, huku baadhi ya taarifa zikisema, Simba itatumia uwanja wowote ulioko Zanzibar kwa sababu yeye pamoja na mpinzani wake wako huko kwenye michuano ya Kombe la Muungano.
Taarifa iliyotolewa Aprili 24, 2026 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ilitangaza mabadiliko ya uwanja wa mchezo namba 169 msimu 2025/26 kati ya Simba na Yanga kutoka Benjamin Mkapa mpaka Meja Jenerali Isamuhyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi huyo alisema, kuhusu kwenda kucheza Isamuhyo, wao hawana pingamizi, watakwenda kucheza mchezo huo kwenye uwanja ambao umepitishwa na TPLB.
Alisema kuwa, hawana sababu ya kupinga kwa kuwa mwenyeji Simba amechagua na Bodi ya Ligi imebariki, huku akitamba kwamba walisajili timu ya kucheza kokote kule msimu huu.
“Maandalizi ya mchezo huo kwenye timu yetu yanaendelea huku tukijinoa na mashindano ya Kombe la Muungano pia ambayo kwetu ni sehemu ya maandalizi.
“Hatutaki kuingia sana huko kwa kuwa leo (jana) timu inacheza mchezo mgumu, lakini kiuongozi vikao rasmi vitaanza leo (jana) kuelekea mchezo huo,” alisema Rodgers.
Rodgers alisema, Yanga haina hofu kabisa kukutana na Simba katika uwanja huo ambao hauna ukubwa kama ulivyo Benjamin Mkapa, lakini hawana shida kwa sababu Bodi ya Ligi imebariki hilo.
“Uwanja wa Isamuhyo hauna shida ya ‘pitch’ (sehemu ya kuchezea) wenye wasiwasi nao ni kutokana na ukubwa wa maeneo ya kuingiza mashabiki wasiozidi 8000.
“Kwa ukubwa wa Dabi mashabiki huwa ni wengi, lakini nafasi pale Isamuhyo ni ndogo ila Yanga itakwenda kupata matokeo mzuri katika mechi hiyo,” alisema.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa uwanja huo kuchezwa mechi kubwa kama Dabi ambayo inatazam-wa na mashabiki wengi kuzidi mechi yoyote Ligi Kuu Bara.