
BANDARI ya Kenya inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Simba, Mkenya Mohammed Bajaber baada ya nyota huyo kupitia kipindi kigumu akiwa na kikosi cha wekundu wa Msim-bazi kutokana na majeraha.
Bajaber aliyejiunga na Simba Agosti 2, 2025, akitokea Kenya Police ya kwao Kenya aliyoipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita chini ya Kocha, Mrundi, Etienne Ndayiragije anayeifundisha TRA United msimu huu, mustakabali wake kwa sasa uko shakani kuelekea msimu ujao.
Ndayiragije, aliyewahi kuifundisha Azam, KMC na Timu ya Taifa ya Tanzania, ameipa ubingwa timu hiyo wa Ligi Kuu ya Kenya 2024-2025, ikiwa ni kwa mara ya kwanza pia katika historia ya kikosi hicho tangu kilipopanda daraja mwaka 2021.
Bajaber alikuwa anasumbuliwa na majeraha akiwa kambini na timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, iliyokuwa inajiandaa na Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN 2024), zilizofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Hata hivyo, wakati akiwa kambini na kikosi hicho, Bajaber aliondoka mapema kabla ya michuano hiyo kuanza Agosti 2, 2025 na kujiunga na Simba, ambapo licha ya dili hilo kukamilika, bado amekumbwa na majeraha ya mara kwa mara.
Taarifa kutoka Kenya, zinaeleza mabosi wa Bandari FC wanaangalia uwezekano wa kumrejesha nyota huyo nyumbani msimu ujao, ikimuhitaji kwa mkopo na sio kumnunua moja kwa moja, jambo linaloweza kufungua mlango kwa nyota huyo kuondoka kikosini.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba siyo Bandari pekee inayomtaka isipokuwa hata waajiri wake wa zamani ambao ni Kenya Police wanaangalia uwezekano wa kumreje-sha nyumbani, japo hadi sasa hakuna pia makubaliano yaliyofikiwa.
“Bajaber ni mchezaji mzuri sana ila rekodi yake ya majeraha ya mara kwa mara inaweza kutishia mus-takabali wake tena kwa msimu ujao, msimu huu ukiisha anabakisha mkataba wa mwaka mmoja, hivyo acha tuone itakavyokuwa,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo mwenye miaka 23, alijiunga na Police FC, Februari 14, 2025, akitokea Nairobi City Stars, akiwa ameshaifungia Simba bao moja tu la Ligi Kuu Bara, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-0, dhidi ya Mbeya City, Desemba 4, 2025.
Bajaber alikuwa nje ya uwanja tangu mara ya mwisho alipoichezea Simba, Januari 18, 2026, katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, ingawa amerejea na sasa anacheza michuano ya Kombe la Muungano inayoendelea Zanzibar.
Katika mechi hiyo ya Januari 18, 2026, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kuisha kwa sare ya bao 1-1, Bajaber alitolewa dakika ya 11, baada ya kukaa chini kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.