
Waziri wa Kilimo wa Iran, Gholamreza Nouri, amesema kuwa mashambulizi na vitendo vya uchokozi vya Marekani vina madhara makubwa kwa usalama wa chakula duniani, na vinatoa kikwazo kikubwa katika kufanikisha lengo la “kutokomeza njaa.”
Nouri alitoa kauli hiyo katika kikao cha pili cha Mkutano wa 38 wa Kanda wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) eneo la Asia na Pasifiki, kilichofanyika Bandar Seri Begawan, Brunei, siku ya Alhamisi.
Amesema kuwa uvamizi wa kijeshi kinyume cha sheria unaofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran umevuruga kwa kiwango kikubwa minyororo ya usambazaji, hasa katika sekta za mafuta, nishati na mbolea, na hivyo kutia doa kubwa katika juhudi za kufikia lengo la “kutokomeza njaa” duniani.
Nouri ameziomba nchi za eneo na mataifa yanayojitegemea kulaani kwa nguvu zote uchokozi wa kijeshi na mzingiro usio halali dhidi ya Iran, akisisitiza haja ya usitishaji wa kudumu na endelevu wa mashambulizi hayo ili kuhakikisha uzalishaji wa kilimo unaendelea bila kukatizwa.
Waziri huyo wa Iran amesisitiza umuhimu wa kukumbatia mikakati ya pamoja ili kubadili mbinu za kilimo na kuimarisha mifumo ya chakula ili iweze kustahimili misukosuko kama hiyo.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Usafirishaji Baharini Iran amesema mzingiro wa bahari uliowekwa na Marekani dhidi ya Iran utaongeza tu mfumuko wa bei duniani, ukosefu wa mafuta, na hasara za kimataifa.