
WAKATI mkataba wa beki wa kati wa KenGold, Faisal Richard Mganga ukifikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu, nyota huyo amesema kwa sasa anapambania kikosi hicho kwa mechi zilizobakia, kisha baada ya hapo ndipo atakaa na kujua hatima yake.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Mbeya City inayoshiriki kwa sasa Ligi Kuu Bara, amesema hakuna mazungumzo yoyote ya kuongeza mkataba mpya na timu hiyo, japo, ataendelea kuipambania kwa nguvu zote kwa maslahi mapana.
“Licha ya kutojua hatima yangu na KenGold ila, sio muda sasa wa kuanza kulizungumzia hilo, baada ya msimu huu kumalizika ndipo nitakapokuwa na wigo mpana wa kuweka wazi kila kitu, kwa sasa malengo yangu ni kufanya vizuri tu,” amesema Faisal.
Beki huyo aliyewahi pia kuichezea Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting, Namungo, Pamba Jiji, Ndanda na Tabora United ambayo kwa sasa ni TRA United, amesema kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu ni ngumu, ila atapambana kwa ajili ya kuibakisha Championship.
KenGold iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, kabla ya mechi ya jana dhidi ya Bigman, inashika nafasi ya tisa na pointi 26, baada ya kushinda saba, sare tano na kupoteza 10, kati ya 22 iliyocheza, huku ikifunga mabao 22 na kuruhusu 27 pia.