
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, amemtaja Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kiongozi aliyeuawa shahidi wa Iran, kuwa ni nembo mapambano, imani na kusimama kidete.
“Tutaendelea kuwa waaminifu kwa ahadi yetu. Tunasimama kidete kutetea kile kiongozi aliyeuawa shahidi wa Jamhuri ya Kiislamu alichosabilia maisha kwa ajili yake na hatutarudi nyuma”, amesema Sheikh Ibrahim Zakzaky katika shughuli ya kumkumbuka Ayatullah Khamenei (RA) iliyofanyika Abuja, mji mkuu wa Nigeria.
Sheikh Zakzaky amesisitiza kuwa: Kuuawa shahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia kumewafichua wanafiki; wale wanaodai kutetea maeneo matakatifu, ilhali wao ni adui. Pia kumeonyesha kwamba kila kitu ambacho Marekani imepeleka katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kinalenga kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu na kusaidia mradi wa kuunda Israel Kubwa.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amesisitiza kuwa: Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran havikuwa dhidi ya nchi moja tu (Iran), bali ni dhidi ya wanadamu wote na watu wote huru; na wale wote wanaopigania haki na uhuru sasa wanajifunza kutokana na vita hivyo.
Wakati huo huo, Gholamreza Mahdavi Raja, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Nigeria, amesema katika mahfali hiyo kwamba: Katika kipindi cha siku arubaini za vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ukweli ulibainika tena kwamba watu wa Iran walisimama imara mbele ya mashinikizo na vitisho. “Leo, baada ya siku hizo arobaini za muqawama na mapambano, tunashuhudia mabadiliko makubwa. Mabadiliko haya si tukio la kisiasa tu; bali ni dhihirisho la nguvu ya taifa”, amesema balozii Mahdavi Raja na kuongeza: Watu wanapotetea haki zao kwa uthabiti, hali halisi inaulazimisha upande wa pili kukubaliana na hali halisi. Siku hizi arobaini zimekuwa uzoefu wa kihistoria. Uzoefu ulioonyesha jinsi umoja wa kitaifa ulivyo na umuhimu mkubwa.