
Arusha. Mahakama ya Rufani nchini, imetupilia mbali rufaa ya madai namba 329 ya mwaka 2024 iliyowasilishwa na warufani watatu wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi.
Mahakama iliridhia kuwa Mahakama Kuu haikukosea katika kutumia mamlaka yake ya kisheria kumuongezea muda mjibu rufaa ili aweze kuwasilisha upya maombi ya mapitio ya kimahakama.
Chanzo cha mgogoro huo kilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Aprili 3, 2024, ambapo jaji aliruhusu ombi la mjibu rufaa la kuongezewa muda wa siku 14 baada ya kubaini kuwa alichelewa kuwasilisha maombi hayo kwa siku 23 kutokana na sababu mbalimbali zilizohusiana na taratibu za kiutawala.
Mahakama kuu iliona kuwa mjibu rufaa alionesha juhudi na ufuatiliaji wa karibu katika kutetea haki zake, hivyo haikuwa sahihi kumzuia kuendelea na hatua za kisheria.
Rufaa hiyo ya madai namba 329/2024 ilikatwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya Pere Muganda.
Hukumu iliyotupilia mbali rufaa hiyo imetolewa Aprili 23, 2026 na majaji watatu ambao ni Barke Sehel, Dk Paul Kihwelo na Profesa Ubena Agatho.
Jaji Kihwelo amesema baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote mbili imeridhia kuwa Mahakama Kuu haikukosea katika kutumia mamlaka yake ya kisheria kumuongezea muda mjibu rufaa ili aweze kuwasilisha upya maombi ya mapitio ya Mahakama.
Warufani, hata hivyo, hawakuridhika na uamuzi huo na waliwasilisha rufaa wakidai kuwa Mahakama Kuu ilikosea kwa kuzingatia mambo yasiyofaa, kupuuza mambo muhimu na kutumia vibaya busara yake katika kutoa uamuzi huo.
Walisisitiza kuwa, ucheleweshaji wa siku 23 ulikuwa mkubwa na haukuwa umeelezewa ipasavyo, hivyo haukustahili kuhalalishwa.
Wakili wa Serikali, aliyewawakilisha warufani, alidai kuwa ili Mahakama iweze kuongezea muda, ni lazima kuwepo na sababu nzuri na ya kutosha kama inavyotakiwa na kifungu cha 14 cha Sheria ya Ukomo.
Kwa mtazamo wake, masharti hayo hayakutimizwa na mjibu rufaa, hivyo Mahakama Kuu ilikosea kutoa uamuzi huo.
Kwa upande wake, wakili wa mjibu rufaa alitetea uamuzi wa Mahakama Kuu akieleza kuwa, mteja wake hakukaa kimya bali alifanya juhudi za dhati kufuatilia haki yake.
Aliongeza kuwa, kucheleweshwa huko kulisababishwa na ucheleweshaji wa kupata nyaraka muhimu pamoja na changamoto za kiutawala, hali iliyokuwa nje ya uwezo wake.
Uamuzi Majaji
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia kumbukumbu za kesi, Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa, hoja kuu ya kuamuliwa ilikuwa ni kama Mahakama Kuu ilitumia vibaya busara yake katika kuongezea muda.
Katika uchambuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa, kifungu cha 14 cha Sheria ya Ukomo kinatoa mamlaka mapana kwa Mahakama kuongeza muda endapo kuna sababu ya msingi na kwamba hakuna tafsiri ya jumla inayoweza kutumika kwa kila kesi.
Mahakama ilisisitiza kuwa, kila kesi inapaswa kuangaliwa kwa mazingira yake ya kipekee na mambo kama juhudi za mwombaji, haraka ya kuchukua hatua na sababu za kuchelewa vinapaswa kuzingatiwa kwa uzito.
Jaji amesema katika kesi hiyo ilibainika kuwa mjibu rufaa alichukua hatua kwa haraka baada ya changamoto alizokutana nazo na hakukaa bila kufanya jitihada.
Aidha, Mahakama ilikataa hoja ya warufani kuwa kucheleweshwa kwa siku 23 kulikuwa kupita kiasi, ikieleza kuwa muda huo haukuwa mkubwa kiasi cha kuondoa haki ya mjibu rufaa, hasa ikizingatiwa kuwa alitoa maelezo ya kuridhisha kuhusu sababu za kuchelewa huko.
Katika hitimisho lake, Mahakama ya Rufaa ilisema wazi kuwa haikuona sababu yoyote ya kuingilia uamuzi wa Mahakama Kuu, ulitolewa kwa kuzingatia sheria na kanuni husika na kuongeza kuwa kumzuia mjibu rufaa kuendelea na shauri lake kungekuwa ni kumnyima haki ya msingi ya kusikilizwa.
“Tumetosheka kwamba Jaji wa Mahakama Kuu alitumia mamlaka yake kwa busara, akizingatia mazingira yote ya kesi hii. Hatuoni sababu ya kuingilia uamuzi huo,” inasema sehemu ya hukumu hiyo.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo kwa gharama, hatua inayomaanisha kuwa warufani watalazimika kulipa gharama za kesi.