
Mwaka 1991, Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au vyama vingi vya siasa, ilibaini dosari nyingi tu katika Katiba ya sasa ya Tanzania ya mwaka 1977 na kupendekeza ifanyiwe marekebisho, badala yake sasa imekuwa donda ndugu.
Mapendekezo hayo ya Tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji mkuu, Francis Nyalali ilitiliwa nguvu na Tume nyingine zilizofuata, lakini leo hii ni miaka 35 inatimia ambapo wahafidhina ndani ya CCM hawataki kusikia mabadiliko ya Katiba.
Hatuwezi kuwa na Katiba ambayo ina vipengele vya kuminya demokrasia kama kuzuia matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani, uwepo wa mgombea huru, Tume kushitakiwa kortini wanapoboronga na uwepo wa Taasisi imara, katikati ya mfumo wa vyama vingi.
Haiwezekani katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, watendaji wa chombo cha kusimamia uchaguzi wateuliwe na Rais ambaye kwa Katiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM), huwa mwenyekiti wa CCM na mgombea wa urais.Tutakaribisha vurugu tu bila kupenda.
Lakini siku zote huwa nasema ukweli una sifa moja kuu, kwamba hata kama ukiukataa namna gani, huwa haugeuki kuwa uongo na sasa Jaji mkuu mstaafu Mohamed Chande, naye amekuja na jambo lile lile, umma unataka Katiba mpya.
Katiba mpya ndio kila kitu, ndio ambayo huzaa taasisi imara (strong constitutions) na Huru kama Bunge, Mahakama, polisi na nyinginezo na ndio ingemzaa mtoto anayeliliwa sana na wadau wa demokrasia, yaani Tume Huru ya Uchaguzi.
Lakini kwa miaka 35 tumekosa utashi wa kisiasa na wahafidhina ndani ya CCM kuhofia Katiba mpya kiasi kwamba sasa kilio hicho kinatajwa kuwa moja ya chanzo cha ghasia zilizotokea siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.
Chanzo ni sababu, asili, chimbuko au mzizi wa suala ambalo limedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na kuwa na athari hasi katika jamii.
Jaji Chande aliongoza Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025, na kugharimu maisha ya watu zaidi 518, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tume ya Jaji Chande, ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zilitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa ilikiwamo la Katiba.
Ripoti inasema yapo masuala ya kisiasa yanayojumuisha madai ya Katiba mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.
Kwa hiyo, kama Serikali inayoongozwa na CCM tangu nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961 ingefanyiwa kazi mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali, pengine haya ya Oktoba 29 yasingejitokeza kwa sababu ni sheria mama na huza sheria zote.
Maana yake ni kwamba tumeacha au kupuuza tatizo tuliloliona tangu mwaka 1991 na kama ni kidonda, basi hadi kikageuka kuwa donda ndugu. Tujitafakari.
Donda-ndugu ni kidonda kinachotokana na damu kuacha kupita katika kiungo kimojawapo cha mwili, husuani katika vidole au katika viungo vya ndani ya mwili kama maini, na kusababisha kiungo hicho kitengeneze kidonda kisichopona.
Wataalamu wa lugha wanaenda mbali na kusema kiungo hicho kisipoondolewa basi kidonda hicho kinasambaa mwili mzima, na kusababisha matatizo mengine makubwa zaidi na ugonjwa wa donda-ndugu hauna tofauti na ugonjwa wa Kansa.
Ndicho kimelipata Taifa letu Oktoba 29,2025 kwa kupuuza maoni ya Watanzania ya muda mrefu juu ya haja ya Katiba yetu ya mwaka 1977 iliyoandikwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, kuandikwa upya kwa mazingira ya sasa.
Naipongeza Tume ya Jaji Chande kuliweka hitaji la Katiba mpya kama moja ya chanzo kilichosababisha vurugu za Oktoba 29 na kuja na mapendekezo yake kwamba ipatikane ipatikane ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa wa mwaka 2029 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.
Tume ikasema kuwa ili kufikia lengo la kupata Katiba kabla ya 2029, basi Serikali iunde Kamati ya Wataalamu wa Katiba ambayo itakuwa na jukumu la kupitia Katiba iliyopo na rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Lakini pia iipitie Katiba Pendekezwa ya Mwaka 2014; ripoti za Tume, Kamati na Vikosi Kazi mbalimbali na baada ya kufanya mapitio ya nyaraka hizo, Kamati ya Wataalamu itapata maoni na michango ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba Mpya itakayopigiwa kura na wananchi.
Nimefurahishwa sana na pendekezo la kuondoa mchakato huo kupita katika Bunge Maalumu la Katiba (BML) kama ilivyokuwa mwaka 2014 ilipohusisha wanasiasa, hasa wabunge na kuweka mbele maslahi ya kisiasa zaidi.
Wajumbe wa BML (wengi wakiwa ni wana CCM), waliliteka Bunge lile na ni kama walitengeneza ‘Parallel draft of constitution’ ambayo iliwaongoza kutoa maoni katika kila sura na ibara kulingana na matakwa ya Chama cha Mapinduzi.
Matokeo yake, yapo mambo ya msingi ambayo watanzania walitaka yawemo yaliondolewa na matokeo yake kukakosekana maridhiano ya kitaifa na kwa vyovyote, Katiba Inayopendekezwa ingekataliwa kwenye sanduku la kura.
Hii ndio pengine ilifanya tusiende kupiga kura ya NDIYO au HAPANA na Serikali ya CCM ikaona isiwe tabu ikaweka mpira kwapani hadi leo kimya.
Pengine ni kwa kutambua kuwa ukishaingiza wanasiasa katika kuamua Sura na Ibara zinazopaswa kuwamo kwa kuzingatia maoni ya wananchi, wataingiza yale tu yenye masilahi ya kisiasa kwao na chama chao na kuwaweka pembeni wananchi na ndio maana Tume ya Jaji Chande inapendekeza wataalamu wa Katiba sio BML.
Mchakato huu ulihakikisha kuwa Katiba ya 2010 iliidhinishwa na Bunge na kuendeshwa na watu, ukiacha rasimu ya 2005, ambayo ilikabiliwa na mizozo mikubwa ya kisiasa Bungeni kabla ya kushindwa katika kura ya maoni.
Majirani zetu Kenya, walianza na Kamati ya Wataalamu (CoE) kwani Sheria iliunda Kamati ya Wataalamu ili kutoa Rasimu ya Katiba Iliyowianishwa, ambayo iliwasilishwa kwa Kamati Teule ya Bunge ya Marekebisho ya Katiba.
Baadaye Bunge lilipitia rasimu, na baada ya maoni na marekebisho ya wananchi, Bunge lilijadili katiba ya mwisho iliyopendekezwa, na hatimaye kuipitisha.
Baada ya kupita katika Bunge la Kitaifa na kupata kibali, rasimu hiyo iliwasilishwa kwa wananchi katika kura ya maoni ya kitaifa Agosti 4, 2010, ambapo ilipitishwa.
Sasa sisi Tanzania, kwa mazingira ya kisiasa tuliyonayo ambapo Bunge la Tanzania lina asilimia zaidi ya 95 ya wabunge wanaotokana na CCM, ni dhahiri kuipeleka Katiba kwa Bunge la aina hiyo itakuwa tunarudi kule kule kwa mwaka 2014.
Ni lazima tutunge sheria ambayo itakuwa shirikishi ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo itaainisha wataalamu hao wa Katiba watapatikanaje na kutoka katika maeneo gani na ni heri wakaomba kazi kuliko kuteuliwa na Rais. Italeta kelele.
Wala Serikali inayoongozwa na CCM isisubiri hitaji la Katiba mpya likavuka na kugeuka kitu kingine kabisa tutatafutana, hiki tulichokiona Oktoba 29,2025 tusitamani kijirudie tena, tuwape watanzania kile wanachokihitaji. Katiba mpya.
Kuzuia hitaji la Katiba mpya ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mikono, yatatafuta njia nyingine ya kupita na hapo ndio hutokea maafa makubwa zaidi. Tutafakari sana kama tuko njia sahihi ya huko tuendako.
Tutafakari tukitambua kuwa Watanzania wa leo na kizazi hiki cha Gen Z, ni tofauti kabisa na kizazi cha umri wa makamu mwenyekiti wa CCM, Steven Wassira, ni kizazi kinachojitambua na kinachoweza kupima mche ni upi na pumba ni zipi.
Tukiingiza propaganda kwenye uhitaji wa Katiba mpya na kutengeneza chawa wa kuhubiri kuwa “Katiba sio kipaumbele chetu,” mjue huko mbele kuna giza. Narudia tena kutahadharisha, kwa upole kabisa, tusisubiri kidonda kikageuka donda ndugu.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900