Uwepo wa wachezaji wa kigeni katika Ligi yoyote ile duniani huwa na faida na hasara zake kuanzia ndani hadi nje ya uwanja.

Faida mojawapo ni kuongeza mvuto na hamasa ya ligi na hata kuimarisha ubora wa timu na ndio maana sio jambo la kushangaza tangu timu zetu zilipoanza kuwa na namba kubwa ya wachezaji wa kigeni, tumeona zikichomoza na kuleta ushindani mkubwa katika mashindano ya klabu Afrika.

Pia jambo lingine ambalo ni faida kutokana na uwepo wa wachezaji wa kigeni katika soka letu hapa Tanzania ni kuambukiza tabia na maisha ya kiweledi kwa wachezaji wetu ambao wengi hawajapitia katika misingi sahihi ya kisoka.

Kinyume na faida hizo, uwepo na ongezeko la wachezaji wa kigeni umeonekana kusababisha hofu kwa wadau wa mpira wa miguu nchini kwamba huenda likawa na athari hasi kwa wachezaji wazawa hasa ile ya kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza jambo ambalo linaweza kusababisha kuporomoka kwa viwango vyao.

Mifano imekuwa ikitolewa ya baadhi ya nyota wazawa ambao walijikuta wakishindwa kupata namba mbele ya wageni kwa nyakati tofauti na kupelekea washindwe kufikia matarajio ya kuwa mastaa wakubwa katika medani ya soka kwa muda mrefu.

Imani hii kwamba wageni wanasababisha kuua viwango vya wachezaji wazawa, imekuwa ikipelekea kundi kubwa la wazawa kuogopa kusajiliwa au kuzikimbia baadhi ya timu kwa kuhofia yanaweza kutokea hayo ambayo wamekuwa wakiaminishwa.

Na imefika hatua kumeibuka maoni kwamba wachezaji wa kigeni wamekuwa wakipewa thamani kubwa tofauti na wazawa hivyo hiyo inachangia kusiwe na uwanja wa usawa na wao wageni kunufaika zaidi na ushauri ambao unatolewa ni kuwapunguza kwa kuamini kwamba wakiwa wachache, wazawa watapata nafasi ya kutosha ya kucheza kulinda viwango vyao.

Hata hivyo ni dhana isiyo na mashiko ambayo wachezaji hapa nyumbani wanapaswa kutoitilia maanani kwani hakuna ukweli wowote kwamba wageni ndio wanasababisha viwango vyao viporomoke.

Kimsingi anguko la wachezaji wazawa linachangiwa na wao wenyewe kutojiandaa kiakili kuhimili ushindani na wageni jambo ambalo linapelekea wapoteze hali ya kujiamini ambayo inachangia kuwafanya wasiwe na ufanisi na mchango mkubwa ndani ya uwanja.

Inawezekana mchezaji mzawa akashinda ushindani dhidi ya mchezaji megni kama atapambana na kuonyesha kiwango bora na nidhamu ya hali ya juu katika viwanja vya mazoezi na pindi anapopata nafasi ya kucheza katika mechi kinyume na hali iliyopo sasa ambapo wengi wamekuwa hawalifanyi hilo tofauti na wageni.

Hakuna kocha ambaye anaweza kuamua tu kutompanga mchezaji mzuri anayeweza kuifanya timu yake ipate matokeo mazuri na kumpa nafasi yule ambaye hana kiwango bora kisa tu utaifa wake au mahali alikotokea.

Hakuna sheria au kanuni ambayo inamlazimisha kocha kupanga mchezaji fulani kwa kuangalia uzawa au ugeni wake na badala yake kinachozingatiwa ni mchango wa muhusika ndani ya uwanja katika kuisaidia timu kufanya vizuri.

Wapo wachezaji wengi wazawa ambao kwa nyakati tofauti wamweza kushinda vita ya ushindani dhidi ya wageni na hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kile ambacho wamekionyesha na sio kutegemea huruma ya utaifa.

Hao wanapaswa kuwa alama ya kuondoa uoga na kutojiamini kwa vijana wazawa hivi sawa ili wapambane kuhakikisha wanalinda nafasi zao katika vikosi vya timu zao badala ya kuweka uoga ambao mwisho wa siku unawaathiri wao wenyewe.

Watumie usajili wa wachezaji wageni kama changamoto ya kuwafanya wapige hatua zaidi badala ya kuwarudisha nyuma.

Wasiingie katika mtego wa kuamini kwamba maendeleo na mafanikio yao yanazuiwa na wachezaji wa kigeni.

Mfano leo hii kila klabu ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaruhusiwa kusajili wachezaji 12 tu wa kigeni kati ya 40 ambao inaweza kuwatumia msimu mzima.

Na kwa bahati nzuri ni timu nne tu ambazo zimekuwa zikisajili wachezajo 12 wa kigeni kila moja huku nyingine 12 zikisajili wachache na baadhi hazisajili kabisa.

Tusiaminishane kwamba hao wachache ni kikwazo kwa wengi kupiga hatua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *