Dar es Salaam. Aliyekuwa mwimbaji wa Konde Music Worldwide, Ibraah, bado moto wake ni uleule kama alivyotambulishwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na lebo hiyo yake Harmonize.
Ibraah, mkali wa kibao cha Nitachelewa (2020), ameendelea kuwapa mashabiki wake muziki mzuri hasa kupitia kifurushi cha Extended Playlist (EP) ambazo amekuwa akiachia kila mara.
Mwimbaji huyo alianza kufahamika baada ya Konde Music kumtambulisha kupitia EP yake, Steps (2020) yenye nyimbo tano, huku akiwashirikisha Harmonize pamoja na wasanii wawili wa Nigeria, Joeboy na Skibii.
Basi kuanzia hapo Ibraah aliendelea kutoa EP na hadi sasa akiwa ni kati ya wasanii wachache wa Bongofleva ambao wamefanikiwa kutoa EP nyingi tena ndani ya kipindi kifupi.
Ni hivi karibuni Ibraah ameachia EP yake mpya, Poison Medicine (PM) (2026) yenye nyimbo tano ambazo zimechanganya mahadhi ya Bongofleva na Afropop.
Kupitia Poison Medicine (PM), Ibraah ameendelea kuthibitisha uwezo wake kama mmoja wa wasanii wanaokua kwa kasi. Hii ni EP iliyojaa hisia na melodi tamu, ikizungumzia mapenzi na maumivu yake, na changamoto za mahusiano. Kwa ujumla hadi sasa Ibraah ameachia EP tano ambazo ni Steps (2020), Karata 3 (2021), Air Piano (2024), Love Season (2025), na Poison Medicine (PM 2026). Huyu ndiye msanii pekee wa Bongofleva aliyeweza kufanya hivyo tangu mwaka 2020, akiwa anafuatiwa kwa ukaribu na staa wa Next Level Music (NLM), Rayvanny mwenye EP nne.
EP za Rayvanny ni pamoja na Flowers (2020), New Chui (2021) na Flowers II (2022), na Unplugged Session (2022) ambayo ilitoka baada ya kuachana na lebo iliyomtoa kimuziki, WCB Wasafi yake Diamond Platnumz.
Kwa upande mwingine, mfululizo huu EP kutokea kwa Ibraah, unaweza kufanishwa na mtindo wa Bosi wake wa zamani, Harmonize ambaye tangu 2020 ameandika albamu tano akiwa ndiye msanii pekee mwenye rekodi hiyo. Itakumbukwa kuwa Ibraah ndiye msanii wa kwanza kusainiwa Konde Music kisha wakafuata wengine kama Country Boy, Cheed, Killy, Anjella na Young Skales kutokea nchini Nigeria.
Hadi anaondoka Konde Music, Ibraah alikuwa ameshirikiana na Harmonize katika nyimbo tano ambazo ni One Night Stand (2020), Addiction (2021), Mdomo (2022), Tunapendeza (2023) na Dharua (2024). Hivyo Ibraah kuwa na mtindo wa kazi unaotaka kufanana na ule wa Harmonize ni jambo la kawaida kwa sababu wamekaa pamoja kwa muda mrefu na kushirikiana katika kazi nyingi. Kati ya wasanii wote waliowahi kupita Konde Music, Ibraah ndiye mwenye EP nyingi, huku wenzake kama Anjella, Killy na Cheed, wakiwa wametoa EP moja moja hadi sasa.
Ibraah alianza safari yake ya muziki tangu akiwa shule ya msingi mkoani Mtwara, ambapo kipaji chake kilianza kuonekana mapema.
Akiwa bado mdogo, aliibuka kuwa msanii bora wa shule, kisha msanii bora wa kata, na mwaka 2014 akafanikiwa kutwaa tuzo ya msanii bora wa wilaya ya Tandahimba, akiwashinda washindani 36 waliokuwa wanawania nafasi hiyo. Mafanikio hayo ya awali yalikuwa ishara ya wazi ya kipaji kikubwa alichokuwa nacho, na baada ya muda, Ibraah alihamia Dar es Salaam kutafuta maisha.
Huko alianza kujishughulisha na biashara ndogo ndogo za umachinga, ikiwemo kuuza CD, maisha haya ya kujituma ndiyo yaliyompa a.k.a ya Chinga. Licha ya changamoto, bado aliendelea kuwa na ndoto kubwa ya kufanya muziki, ingawa hakujua pa kuanzia wala njia sahihi ya kufikia mafanikio hayo. Lakini aliposikia kuwa Harmonize amefungua lebo, Ibraah alianza kutafuta nafasi ya kusainiwa.
Harmonize alivutiwa na kipaji cha Ibraah na hatimaye akakubali kumsaini chini ya Konde Music, na hapo ndipo ndoto ya Ibraah ilianza kutimia rasmi, na safari yake ya muziki ikaanza na sasa akiwa na EP zake tano mkononi. Mbali na EP, Ibraah akiwa Konde Music aliachia albamu moja, The King of New School (2022) yenye nyimbo 17 huku akiwashirikisha wasanii kama Maud Elka, Christian Bella, Roberto na kadhalika.
Ikumbukwe Harmonize alitangaza rasmi kuanzisha Konde Music hapo Oktoba 10, 2019, ikiwa ni kipindi kifupi baada ya kujitoa WCB Wasafi, lebo ambayo ilimtoa kimuziki kupitia wimbo wake, Aiyola (2015) uliotayarishwa na Maxmizer.