
Viongozi wa wanamgambo wa Sudan wanaojulikana kwa jina la Kikosi cha Msaada wa Haraka au Rapid Support Forces (RSF) na mtandao wao wamekusanya mamilioni ya mali za kifahari huko Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Sentry, kundi la uchunguzi la Marekani, umeonyesha kuwa watu wenye mfungamano na wanamgambo wa RSF, wakiongozwa na kamanda wao, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, wamejilimbikizia mali za kifahari huko Dubai zenye thamani ya pauni milioni 17.7.
Kundi la Sentry limefichua haya huku Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ukituhumiwa kulifadhili kifedha kundi la wanamgambo wa RSF wa Sudan wanaotuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki nchini humo.
Ripoti ya kundi la uchunguzi la Sentry la Marekani imefichua kuwa Imarati inafanya kazi kama kitovu muhimu cha kuhifadhi mali na shughuli za kifedha zinazohusishwa na kundi la wanamgambo wa RSF huku kundi hilo likijiimarisha kijeshi na kiviwanda barani Afrika na Asia Magharibi.
Uchunguzi wa Sentry umesisitiza kuwa UAE inafanya kazi kama “mahali usalama” kwa viongozi wa RSF na jamaa zao, na pia kwa utajiri unaotokana na dhahabu iliyoibwa ya Sudan.
Baada ya kunyakua mgodi mkubwa zaidi wa dhahabu wa Darfur mwaka 2017, Hemedti na mtandao wake waliripotiwa kutumia kampuni za Imarati kuuza dhahabu haramu, na hivyo kupata fursa ya biashara ya dhahabu inayokua ya Dubai.