Dar es Salaam. Ni faraja kwa wasichana wa rika balehe na wanawake wadogo walioondoka nje ya mfumo rasmi wa elimu kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ujauzito, baada ya Taasisi ya Doris Mollel kujipanga kutekeleza mradi wa kusaidia kundi hilo kurejea shule katika mikoa 15 ndani ya halmashauri 47.
Mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Global Fund utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita nchini kuwawezesha wasichana balehe na wanawake wadogo waliokatisha shule kwa changamoto mbalimbali kurejea shuleni, pamoja na kuwapeleka kwenye nyumba salama wale wanaokimbia matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye makazi yao.
Pamoja na hayo, Taasisi ya Doris Mollel imesema mradi huo utawezesha kushawishi baadhi ya halmashauri kuwa za mfano katika utoaji wa taulo kwa wasichana mashuleni.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, Doris Mollel akielezea namna watakavyotekeleza mradi wa kuwarejesha wasichana wa rikabakehe shule baada ya kukatisha kutokana na ujauzito
Yote hayo yameelezwa jana Jumanne, Aprili 28, 2026 kwenye kikao kazi cha wadau na maofisa wa Serikali waliokutana kujadili namna ya kutekeleza mradi huo na kuleta matokeo chanya kwenye jamii na uendelevu wake baada ya ufadhili wa mradi kutamatika.
Akifungua kikao hicho, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji Wizara ya Afya, Paul John, amesema wizara hiyo inatambua na kuthamini michango ya wadau katika utoaji wa huduma za Ukimwi na afua zingine.
“Afua hii ni muhimu kwa ulinzi wa mtoto, sisi kama Wizara ya Afya tunafahamu eneo la wasichana wa rika balehe bado liko nyuma katika kukabili maambukizi na linaongoza kwa maambukizi.
“Kundi hili ndilo linaongoza kwa maambukizi ya Ukimwi na hivyo mikakati mikubwa isipotengenezwa ya kuhakikisha ulinzi wa msichana, Taifa litaangamia na hakutakuwa na Taifa la kesho,” amesema.
Amesema kupitia mradi huo ni muhimu nguvu zaidi ikawekezwa kwa kundi la wasichana balehe na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano.
Kuhusu uanzishwaji wa nyumba salama, amesema nalo ni eneo muhimu kwani wapo watoto wanaofanyiwa ukatili na hawana pa kukimbilia, hivyo nyumba hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa waathirika wa matukio ya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Elias Masangora, amesema wasichana balehe na wanawake wadogo wapo kwenye hatari kubwa ya kukumbana na changamoto kutokana na kujaribu mambo mbalimbali.
“Tukifika kwenye halmashauri hizi 47 na kwenye mikoa 15 tutalifikia kundi kubwa, pamoja na kwamba wizara imetoa waraka wa kuwarudisha watoto wanaopata ujauzito shuleni, bado jamii haijapata elimu ya kutosha. Sasa ni wakati wa mradi huu kusaidia watoto wenye ujauzito kurudi shuleni,” amesema.
Amesema kwa kuwa mradi huo ni mfupi, ni muhimu kutafakari shughuli ambazo zitakwenda kugusa kundi la wasichana balehe na wanawake wadogo.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sara Sanga amesema wizara hiyo inafanya kazi kwa karibu na wamiliki wa makao na nyumba salama na hadi sasa wamesajili makao 426 na nyumba salama 19.
“Kutokana na umuhimu wa jambo hili, Serikali imetambua na tuna mradi wa pamoja uliodhaminiwa na Benki ya Dunia wa ujenzi wa nyumba zingine 10, niipongeze taasisi ya Doris Mollel kwa kuona umuhimu wa huu mradi wa kuwatambua watoto wenye uhitaji katika halmashauri 47 na tunawahakikishia ushirikiano,” amesema.
Akizungumzia mradi wa kuwezesha wasichana balehe na wanawake wadogo, Meneja Miradi Tume ya Huduma kwa Jamii ya Kikristo (CSSC), Dk Karugira Rweyemamu, amesema mradi huo unalenga vijana wa kike wa rika balehe na wanawake wadogo Tanzania, hasa kuwarudisha shule watoto wa kike waliokatisha masomo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito.
Kundi lingine ni kutoa hifadhi bora ya nyumba salama kwa kundi la watoto wa kike walio kwenye mazingira yasiyo salama katika wilaya 47 za Tanzania.
“Mradi huu umekuja wakati muafaka, tangu tulipotangaziwa kuwa UKIMWI ni janga kumekuwa na jitihada za kupunguza maambukizi mapya, japo kundi la watoto wa rika balehe maambukizi bado ni changamoto,” amesema.
Meneja Miradi Tume ya Huduma kwa Jamii ya Kikristo (CSSC), Dk Karugira Rweyemamu akizungumza katika kikao maalumu iliyowashirikisha wadau mbalimbali kujadili namna ya kutekeleza mradi wa kuwarejesha shule wasichana wa rika balehe
Dk Rweyemamu amesema mradi huo utakwenda kutoa majawabu ya namna ya kushughulikia tatizo la maambukizi kwa vijana kwa njia ya tiba kuzuia maambukizi mapya.
Amesema mradi huo utakuwa tumaini kwa kundi hilo la vijana kuwa na afya bora na kuona kesho yao ikiwa njema.
Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation (DMF), Doris Mollel amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuandaa mikutano zaidi ya minne kila mwaka yenye lengo la kujadili namna ya kutatua changamoto kwa vijana.
“Kupitia jukwaa hili na mashirika zaidi ya 100 huwa tunakutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo vijana na namna ya kuzitatua, ikiwemo upatikanaji wa vyombo rafiki kwa vijana, upatikanaji wa bidhaa za watoto wa kike kwa gharama nafuu na watoto wa kike waliopata ujauzito wanaotamani kurudi shule lakini wameshindwa,” amesema.
Amesema kupitia mradi wanaokwenda kuutekeleza kwa kipindi cha miezi sita ukifadhiliwa na Shirika la Global Fund, watashawishi halmashauri kuwezesha watoto wa kike kupata taulo.
Doris amesema mradi huo utatekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini na watashirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha mradi huo aliouita wa matumaini.
“Mtoto wa kike atakayeguswa na mradi huu tunakwenda kurudisha tumaini la maisha yake tena, lakini pia kwa namna ambavyo hizi nyumba salama zinakwenda kutunza utu wa mtoto wa kike ni jukumu letu kuhakikisha watoto wa kike wanaishi kwenye maisha bora,” amesema.