Nchini Mali, kundi la wanajihadi la JNIM linaendelea na tishio lake la kuzingira mji wa Bamako, kufuatia mashambulizi yasiyo ya kawaida ya wanajihadi hao na waasi yalipiga moyo wa utawala huko Kati, karibu na mji wa Bamako, ambapo Waziri wa Ulinzi aliuawa. Mashambulizi pia yamerekodiwa ndani ya nchi, ambapo jeshi limepoteza udhibiti wa miji kadhaa ya kimkakati na hivyo kutekwa na waasi.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Sasa, kizuizi kinaimarishwa kuzunguka mji mkuu. Tangu siku ya Jumatano, barabara kadhaa zimekatwa au kuharibiwa vibaya.

Upande wa magharibi, barabara inayotoka Bamako kuelekea Kéniéba, imefungwa. Huko Sorybougou, chini ya kilomita 80 kutoka mji mkuu wa Bamako, mamia ya magari yamekwama: malori, mabasi, na magari. Ndani ya magari hayo, abiria ambao wanaonekana wamechoka wamekwama kwa saa nyingi na hawana msaada wowote.

Dereva mmoja anashuhudia: “Walitusimamisha hapa Sorybougou. Wanasema hakuna magari yanayoweza kuondoka kwenda Bamako. Bado tuko hapa: kuna mabasi na magari mengine mengi, magari makubwa ya mizigo, pamoja na malori yanayobeba mkaa. Kuna zaidi ya magari 1,000 hapa. Miongoni mwao, angalau mabasi 80 ya abiria. Kuna abiria wengi, wametawanyika msituni. Hawana hata maji ya kunywa. Hawajamshambulia mtu yeyote, wamefunga tu barabara. Hata pikipiki haziwezi kupita. Magari yanayotoka Bamako yanaweza kupita, lakini yale yanayotaka kuingia Bamako, haiwezekani.” »

“Suluhisho pekee ni kurudi nyuma”

Katika sehemu hiyo ya barabara, wengine wanapendelea kurudi nyuma, kama msafiri huyu ambaye hakutaka jina lake litajwe: “Tuliondoka Kéniéba kwenda Bamako. Tulipita Kita na kufika Néguéla. Huko, tuliarifiwa kwamba barabara imefungwa na haiwezekai kwenda Bamako. Suluhisho pekee ni kurudi nyuma. Kwa kweli, ni hali ya kutisha sana.”

Kusini, hali hiyo inajitokeza kwenye barabara ya Sikasso. Huko Ouélessébougou, JNIM inaweka vizuizi vikali kwa magari yote yanayoelekea Bamako. Kulingana na mtu aliyetaka kusafiri hadi mji mkuu wa Mali, basi lake, ambalo lilikuwa limeondoka kutoka mji wa Bougouni, lilifika karibu na Keleya, kilomita 100 kusini mwa Bamako, ambapo wapiganaji wa JNIM walimlazimisha dereva kurudi nyuma.

Kwa upande wa mashariki, barabara inayotoka Bamako kuelekea Kourémalé pia imefungwa. Kulingana na chanzo kingine tulichowasiliana nacho, mamia ya magari yalizuiliwa Jumatano na JNIM huko Naréna, mji ulioko kwenye barabara hii. Kwenye barabara inayotoka Bamako kuelekea Ségou, madereva wa magari ya uchukuzi wanazoea hali hiyo. Wanazunguka eneo lililofungwa, wakielekea msitu wa Faya, wakipita kwenye daraja la Kayo kwenye barabara ya Koulikoro, na hatimaye wanaingia mjini Bamako.

Kulingana na taarifa zetu, wanajihadi wanawaruhusu wakazi wa Bamako kuondoka, lakini wanawazuia kuingia katika mji huo. Hata hivyo tunaweza kuthibitisha kwamba baadhi ya mabasi, yaliyokwepa barabara kuu na kutumia barabara za msituni, yaliweza kufika Bamako siku ya Jumatano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *