Kibaha. Wafanyakazi mkoani Pwani wameeleza malalamiko yao juu ya kuendelea kwa changamoto walizowasilisha katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka jana, wakidai kuwa hadi sasa hazijapatiwa ufumbuzi, hali inayochochea vitendo vya ukandamizaji kazini hususan katika sekta binafsi.

Wakizungumza leo Mei 1, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa wilayani Bagamoyo, wafanyakazi hao wamesema baadhi ya waajiri katika kampuni binafsi bado wanakiuka sheria za kazi bila kuchukuliwa hatua stahiki.

Changamoto hizo ziliwasilishwa kupitia risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Pwani, iliyosomwa na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Pwani, Susan Shesha. Amesema bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi, hasa katika sekta binafsi.

Picha matukio maadhimisho Mei Mos Pwani 2026

Ameeleza kuwa baadhi ya waajiri hawatoi mikataba rasmi, hawalipi mishahara inayokidhi viwango elekezi vya Serikali, na huwanyima wafanyakazi haki ya likizo, hali inayokiuka sheria za kazi.

“Baadhi ya makampuni hayawapi mikataba wafanyakazi wao, hawawapi likizo na mishahara wanayolipwa haikidhi viwango vilivyowekwa,” amesema.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mfanyakazi Anna Leon ambaye amesema; “Ni jambo la kusikitisha kuwa yale tuliyoyalalamikia mwaka jana ndiyo yanajirudia mwaka huu. Bado hatuna mikataba ya uhakika, mishahara haikidhi viwango na haki zetu zinapuuzwa.”

Mfanyakazi mwingine, Hadija Salumu amesema kinachoumiza zaidi ni kuona kuwa hata kampuni yaliyotajwa awali kwa kukiuka sheria bado yanaendelea na vitendo hivyo bila mabadiliko yoyote.

“Hii inaonyesha wazi kuwa hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Wafanyakazi tunaendelea kuteseka huku tukitegemea sauti zetu zisikike,” amesema.

Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuahidi kuchukua hatua madhubuti kuzitatua.

Amesema ofisi yake itaangalia uwezekano wa kuimarisha mifumo ya kisheria, ikiwemo kuweka masharti mahsusi katika mikataba ya uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wote wanazingatia haki na masilahi ya wafanyakazi.

“Hatutakuwa tayari kuona wawekezaji wanakuja Pwani kisha wanakiuka haki za wafanyakazi. Tutahakikisha mikataba ya uwekezaji inabeba vipengele vinavyolinda wafanyakazi na kuwa na nguvu ya kisheria ili hatua zichukuliwe kwa wanaokiuka,” amesema Kunenge.

Ameongeza kuwa amezipokea changamoto zilizowasilishwa na kuahidi kuwa zitafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa kulinda haki za wafanyakazi ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *