Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani watumishi wa umma 10, akiwamo hakimu, pamoja na wafanyabiashara wanne, kwa tuhuma za kuhusika katika ubadhirifu wa zaidi ya Sh261 milioni za fedha za mirathi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 30, 2026 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge, uchunguzi uliofanywa umebaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha hizo uliotokea katika akaunti ya mirathi ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita.

“Watumishi sita wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita walihusika moja kwa moja katika ubadhirifu huo kwa kuwalipa watu wanane ambao hawakuwa na madai yoyote ya mirathi mahakamani,”amesema Ruge.

Amesema lengo la malipo hayo lilikuwa kurejesha fedha hizo kwa njia ya ‘kick back’ kwa watumishi hao kwa wenza wao  kupitia miamala ya benki na mitandao ya simu, kinyume cha utaratibu.

Watumishi wa mahakama wanaotajwa katika tuhuma hizo ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Veronica Mwanasenga (Ofisa Hesabu Mkuu), Bulemo Mswaga (Msaidizi wa Hesabu), Mercy Magezi (Mhasibu), Baldo Kafene (Msaidizi wa Kumbukumbu), Emma Matabaro na dereva kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, William Mbwambo.

Aidha, uchunguzi huo umehusisha pia watumishi wengine wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali, akiwamo tabibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Upendo Rugohe.

Pia, wamo mtumishi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Felix Swaty; mhaidrolojia kutoka Wizara ya Maji, Dodoma, Salimu Lyimo na Diwani wa Kata ya Majengo, Monduli mkoani Arusha, Mgema Julius.

Wafanyabiashara wanaotajwa katika shauri hilo ni Amani Abdallah, Erick Chitumbi, Michael Chanzi na David Mrope.

Takukuru imesema baada ya kukamilika kwa uchunguzi na kupatikana kibali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), watuhumiwa wote walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita Aprili 30, 2026.

Mashauri matano ya uhujumu uchumi yamefunguliwa dhidi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *