
Mbeya. Wizara ya Afya imezindua kamati ya ushauri na usajili wa takwimu za visa vya wagonjwa wa saratani katika Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH).
Hatua hiyo imetajwa kuwezesha wataalamu kupata takwimu sahihi za wagonjwa zitakazosaidia kuboresha huduma na utungaji wa sera za matibabu nchini.
Kamati hiyo imezinduliwa Aprili 30, 2026, na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD), kutoka Wizara ya Afya, Edith Bakari katika Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Amesema kuwa mfumo wa ukusanyaji takwimu unakwenda kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa taarifa sahihi katika vituo vya afya za msingi.
“Mbali na mafanikio katika Hospitali za Kanda za mikoa bado kuna pengo la taarifa kutoka vituo vya afya za msingi,” amesema.
Edith amesema kuwa uwepo wa kamati hiyo inakwenda kuhakikisha takwimu zinakusanywa kwa ubora kwa lengo kusaidia katika kupanga sera sahihi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH), Dk Lazaro Mboma amesema wana kila sababu kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo kubwa ambayo itakuwa mwarobaini wa upatikanaji wa takwimu sahihi za wagonjwa wa saratani nchini.
“Uzinduzi wa kamati hii umekuja wakati mwafaka ambapo MZRH, inaenda kutoa na kuboresha huduma za kibobezi kwa wagonjwa wa saratani.
“Tunashukuru Wizara kwa hatua hii muhimu ,lakini tutatoa elimu wananchi wajue uwepo wa huduma bobezi za saratani kufuatia Serikali kuwekeza vifaa tiba na wataalam bobezi katika hosptali ya Kanda,” amesema.
Naye Mratibu wa magonjwa yasiyoambukizwa Mkoa wa Mbeya, Dk Reinfridy Chombo, amesema uzinduzi wa kamati hiyo ni hatua kubwa ya kufanya maboresho ya utoaji wa huduma bora na kupata takwimu sahihi.
Aidha amewataka wataalamu kwenye kamati hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kuwezesha Serikali kupanga mipango thabiti ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkazi wa Soko Matola jijini hapa, Asha Jumaa amesema hatua hiyo itarahisisha wagonjwa wa saratani wanao bainika kupata huduma bora na kurahisisha ufuatiliaji.