
Kajuna FC ya Kigoma imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) 2026, baada ya leo Jumamosi, Aprili 2, 2026, kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kahama Madini ya Shinyanga kwenye mechi ya fainali iliyochezwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Mabao ya Kajuna katika mchezo wa leo yamefungwa na Yusuph Kakoko katika dakika ya 60 na Abas Haruna dakika ya 66.
Mbali na taji ambalo Kajuna imepata, timu hiyo imeonekana kutawala tuzo binafsi za mashindano hayo huku timu nyingine zikiambulia patupu.
Tuzo ya Mchezaji Bora wa mashindano imechukuliwa na Kakoko ambaye pia ameibuka Mfungaji Bora, huku Kipa Bora akiwa ni Evance Umba naye wa Kajuna.
Aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa mashindano hayo ni Habibu Kondo anayeinoa Kajuna huku timu yenye nidhamu ikiwa ni FGA Talents ya Morogoro.
Mshindi wa tuzo ya Refa Bora wa mashindano ni Hassan Abri wa Iringa na Mwamuzi Bora Msaidizi ni Seleman Ayoub wa Arusha.
Katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu, Mount Hanang ya Manyara imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand Masasi FC ya Mtwara.
Bao pekee la Mount Hanang katika mechi hiyo limefungwa kwa mkwaju wa penalti na John Urassa katika dakika ya 72.
Kajuna na Kahama Madini zilizocheza mechi ya Fainali, zote zimefuzu First League huku Mount Hanang na Stand Masasi zikisubiria kucheza mechi za mchujo kuwania nafasi nyingine mbili za kupanda ligi hiyo.