
USS Gerald R. Ford, meli kubwa zaidi ya kivita na ya gharama ya juu kuwahi kuundwa na Marekani, imelazimika kujiondoa kutoka ukanda wa Asia Magharibi baada ya siku 309 za operesheni endelevu baharini, ikiwa katika jukumu la kuunga mkono vita dhidi ya Iran.
Chombo hicho cha kivita chenye thamani ya dola bilioni 13 na chenye uwezo wa kubeba idadi kubwa ya ndege za kivita sasa kinarejea Norfolk, Virginia, kikiwa katika hali ya uchakavu mkubwa wa kiufundi—hatua inayotafsiriwa na wachambuzi wa kijeshi kama kurudi nyuma kwa aibu, ikifichua udhaifu ndani ya mashine ya vita ya Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Press TV, kuondoka kwa USS Gerald R. Ford, kunakotarajiwa katikati ya Mei 2026, kunaacha uwepo wa kijeshi wa Marekani baharini ukiwa umedhoofika katika wakati nyeti wa kimkakati. Ingawa manowari nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba ndege za kivita—USS George H.W. Bush na USS Abraham Lincoln—zinaendelea kuwepo ili kutekeleza mzingiro wa baharini dhidi ya usafirishaji wa mafuta wa Iran, pengo lililoachwa na Ford linapunguza uwezo wa mashambulizi ya haraka, hasa wakati juhudi za kidiplomasia kati ya Washington na Tehran zimekwama kabisa.
Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, amekiri mbele ya Bunge tarehe 29 Aprili kwamba uamuzi wa kuongeza muda wa operesheni ya Ford ulikuwa “mgumu sana,” kauli ambayo wachambuzi wanaiona kama ishara ya wazi kuwa Marekani imejitanua kupita uwezo wake katika mzozo huo.
Operesheni ya siku 309—ikiwa ndiyo ndefu zaidi tangu enzi za Vita vya Vietnam—imeathiri vibaya uwezo wa meli hiyo kubwa ya kivita. Mnamo Machi 2026, moto ulizuka katika eneo la kufulia ndani ya manowari hiyo, ukisababisha majeruhi miongoni mwa mabaharia na kuwahamisha zaidi ya wafanyakazi 600 kutoka maeneo yao ya kulala.
Kwa mtazamo wa wachunguzi wa kijeshi wa ukanda wa Bahari ya Hindi, kujiondoa kwa USS Gerald R. Ford kunatuma ujumbe usiofichika kwa dunia: licha ya mbwembwe na uwekezaji mkubwa wa fedha, uwezo wa kijeshi wa Marekani unaanza kulemewa na mzigo wa operesheni zake zenyewe.