KATIKA Dabi ya Kariakoo siyo ajabu kuona mambo yasiyotegemewa yakitokea uwanjani na hata nje ya uwanja. Kuna nyakati ambazo mechi huanza kwa kasi ya kawaida, lakini ghafla hubadilika na kuwa na matukio ya kushangaza yanayoweza kubadili kabisa mwelekeo wa mchezo.

KADI NYEKUNDU ZA GHAFLA

Moja ya matukio yanayokumbukwa ni yale ya kadi nyekundu za ghafla ambazo hutolewa katika mazingira ya utata. Wachezaji wamekuwa wakitolewa nje kwa makosa ambayo wakati mwingine huonekana madogo, lakini kutokana na presha ya dabi, waamuzi hulazimika kuchukua uamuzi mgumu.

Dabi ya mwaka 2017 ilishuhudia mchezaji wa Simba Janvier Besala Bokungu, akionyeshwa kadi nyekundu mapema kipindi cha pili, jambo lililobadili kabisa mwenendo wa mchezo na kuipa Yanga nafasi ya kutawala dakika zilizobaki.

MABAO YA DAKIKA ZA MWISHO

Pia kumekuwa na matukio ya mabao ya dakika za mwisho yanayobadilisha kila kitu. Timu ikiwa inaonekana kushinda au kutoka sare, ghafla bao la dakika za majeruhi huingia na kuamsha shangwe au majonzi makubwa.

Mwaka 2020, Yanga ilisawazisha bao dakika za nyongeza baada ya Simba kuongoza kwa muda mrefu, bao hilo likiwa gumzo kubwa kutokana na muda liliofungwa. Katika Dabi ya Kariakoo ya Januari 4, 2020, Yanga ilifanya comeback ya kusisimua baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0. Ndani ya dakika nne tu, Mapinduzi Balama na Mohamed Banka waliisawazishia timu hiyo, kabla ya mchezo kumalizika kwa sare ya 2-2, matokeo yaliyochukuliwa kama ushindi kwa upande wa Yanga kutokana na namna walivyorejea mchezoni.

VURUGU ZA MASHABIKI

Mbali na hilo, dabi imewahi kushuhudia matukio ya vurugu kutoka kwa mashabiki, hasa pale matokeo yanapokwenda tofauti na matarajio yao.

Katika dabi ya Oktoba 1, 2016, mashabiki waliwahi kurusha vitu uwanjani na kusababisha mchezo kusimama kwa muda kabla ya kuendelea, sababu ya vurugu ni mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, alifunga bao la kwanza (dakika ya 26) ambalo mashabiki na wachezaji wa Simba walidai alishika mpira kabla ya kufunga.

Kadi Nyekundu:Baada ya bao hilo, nahodha wa Simba, Jonas Mkude, alipewa kadi nyekundu kwa kumlalamikia mwamuzi Martin Saanya kwa hasira. mashabiki wa Simba walikasirishwa na maamuzi hayo na kuanza kung’oa viti na kuvirusha uwanjani.

MAKOSA YA AJABU UWANJANI

Kuna nyakati ambapo wachezaji wamejikuta wakifanya makosa ya ajabu kabisa uwanjani, kama vile kujifunga wenyewe au kukosa nafasi za wazi za kufunga mabao.

Dabi ya mwaka 2018 iliwahi kushuhudia katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti 22, 2018, ambapo aliyekuwa beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alijifunga bao lililozua mjadala mzito. akijifunga bao la kizembe wakati akijaribu kuokoa hatari, tukio lililowapa ushindi wapinzani wao na kuacha maswali mengi kwa mashabiki.

BENCHI LA UFUNDI KUCHAFUKA

Si hivyo tu, hata benchi la ufundi limewahi kuingia kwenye matukio ya kushangaza. Makocha wameonekana wakilalamika kwa jazba, wengine wakionyeshwa kadi au hata kuingia uwanjani kupinga maamuzi.

Kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, aliwahi kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 25, 2021 baada ya kulumbana na mwamuzi. Licha ya tukio hilo, Yanga ilishinda mchezo huo kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Mayele.

MAZINGIRA YA UWANJA

Katika baadhi ya matukio, hali ya hewa au mazingira ya uwanja nayo imewahi kuwa sehemu ya ajabu ya dabi. Mfano mzuri ni dabi ya Aprili 20, 2024, ambapo mvua kubwa ilinyesha katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kusababisha baadhi ya maeneo kuwa na madimbwi ya maji. Licha ya hali hiyo, mchezo uliendelea na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

VAR NA MABISHANO

Pia, teknolojia ya VAR ilipoanza kutumika imeongeza sura mpya ya matukio ya ajabu kwenye dabi.

Katika baadhi ya mechi, maamuzi ya mabao kubatilishwa au kucheleweshwa yametokana na VAR na kuibua mijadala mikubwa. Katika dabi ya Machi Mosi, 2026 iliyochezwa Zanzibar, VAR haikutumika licha ya matarajio ya mashabiki.

Hali hiyo ilisababisha mjadala mkubwa baada ya bao la Simba lililofungwa na Seleman Mwalimu kukataliwa kwa madai kuwa aliotea, jambo lililozua gumzo mitaani na mitandaoni.

Kwa ujumla, dabi ya Kariakoo imekuwa ikijengwa na matukio mengi ya ajabu yanayoifanya kuwa tofauti na mechi nyingine. Ni mchezo unaobeba hisia kali, ushindani mkubwa na wakati mwingine mambo yasiyotabirika.

Kila unapochezwa, mashabiki husubiri si tu kuona nani ataibuka mshindi, bali pia ni tukio gani jipya la kushangaza litatokea na kuandika historia nyingine ndani ya dabi hii kubwa zaidi Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *