Unguja. Wakati mkutano wa tatu wa baraza la 11 la wawakilishi ukianza kesho, Mei 6, 2026, wananchi na wadau mbalimbali wameeleza matarajio yao, wakisisitiza umuhimu wa wawakilishi kujikita katika mijadala yenye maslahi ya umma, hususan kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kwa takribani mwezi mmoja na nusu hadi Juni 23, 2026, na moja ya ajenda kuu itakuwa kujadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Mbali na mjadala wa bajeti, baraza hilo pia linatarajia kupokea na kujadili miswada miwili ya sheria, ikiwamo Muswada wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Sheria ya Makadirio ya Matumizi.

Aidha, wajumbe watajadili taarifa ya Serikali kuhusu hali ya dawa za kulevya Zanzibar kwa mwaka 2024.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza, Othman Ali Haji, kwa niaba ya Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Msellem, jumla ya maswali 506 yatajadiliwa katika mkutano huo. Kati ya hayo, maswali 459 ni mapya na 47 yamebaki kutoka mkutano uliopita.

“Huu ni mkutano wa bajeti, hivyo utahusisha mjadala wa bajeti kuu ya Serikali pamoja na bajeti za kisekta, sambamba na shughuli nyingine kwa mujibu wa kanuni za Baraza,” amesema.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakadiriwa kufikia Sh8.217 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh1.235 trilioni, sawa na asilimia 17.69 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliotangulia ya Sh6.982 trilioni.

Maoni ya wananchi

Baadhi ya wananchi na wachambuzi wa masuala ya kijamii wamesema ni muhimu kwa wawakilishi kutumia nafasi hiyo kuisimamia Serikali ipasavyo, badala ya kujikita katika masuala binafsi.

Ofisa mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Enzi Talibu, amesema wawakilishi wanapaswa kuzingatia zaidi sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi, kama maji, barabara, elimu na huduma za kijamii.

“Tunatarajia wawakilishi waibane Serikali. Gharama za maisha zimepanda na wananchi wengi wanapata ugumu hata kumudu milo miwili kwa siku. Hatujaona mikakati thabiti ya kukabiliana na hali hii,” amesema.

Ameongeza kuwa tatizo la maji Zanzibar limeendelea kwa zaidi ya miongo mitatu bila kupatiwa suluhisho la kudumu, huku akisisitiza umuhimu wa Serikali kuweka vipaumbele katika utekelezaji wa miradi.

“Ni vyema kupunguza miradi mingi inayotekelezwa kwa wakati mmoja wakati mapato ni madogo, na badala yake kuelekeza nguvu kwenye huduma muhimu kama maji, barabara na afya,” amesisitiza.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kijamii, Ali Makame, amesema changamoto ya maisha ni ajenda kuu inayopaswa kupewa uzito katika mkutano huo, hasa kwa kuzingatia wananchi wa kipato cha chini.

Ametaja pia umuhimu wa kuimarisha sekta ya kilimo, ikiwamo kupitia upya ruzuku za pembejeo na kuweka mikakati ya kuinua mazao ya kimkakati kama karafuu na nazi, ambayo kwa miaka ya nyuma yalikuwa mhimili wa uchumi wa Zanzibar.

“Sekta za afya, makazi bora na elimu bado zinahitaji mipango madhubuti ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi,” amesema.

Naye Mwasshamba Jabir Issa, mkazi wa Jang’ombe, amesema baadhi ya wawakilishi hawatembelei majimbo yao mara kwa mara, hali inayochangia kushindwa kuwasilisha ipasavyo changamoto za wananchi.

“Wananchi wanapitia hali ngumu, lakini wanaopaswa kuwasemea hawafiki mara kwa mara kusikiliza matatizo yao. Tunatarajia safari hii wawakilishi watajadili ajenda zenye maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema.Bottom of Form

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *