Dodoma. Wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi mkoani Dodoma wamepewa siku 14 kulipa madeni yao, huku mamlaka zikionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaoshindwa kutekeleza wajibu huo ndani ya muda uliowekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne, Mei 5, 2026, jijini Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Geofrey Mwamsojo, amesema ofisi yake imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha ukusanyaji wa kodi hiyo unafikia malengo ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema wadaiwa wote wanapaswa kulipa kodi ya pango la ardhi ndani ya siku 14 tangu kupokea ankara au taarifa rasmi, akibainisha kuwa kutokufanya hivyo kutasababisha hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani, kutozwa adhabu pamoja na kubatilishiwa umiliki wa ardhi.

Kwa mujibu wa Mwamsojo, hadi sasa Mkoa wa Dodoma umefanikiwa kukusanya Sh17.5 bilioni kati ya lengo la Sh23 bilioni, sawa na asilimia 76.5, hali inayoonesha mwenendo mzuri, ingawa bado kuna haja ya kuongeza juhudi ili kufikia asilimia 100.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Geofrey  Mwamsojo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makusanyo ya kodi ya ardhi, kushoto ni Ofisa Ardhi mteule Mkoa wa Dodoma, Letire Shoo, kulia ni Ofisa Ardhi Jiji la Dodoma, Matilda  Mactavo.

“Natoa wito kwa wadaiwa wote kulipa kodi ya pango la ardhi ndani ya siku 14 tangu kupokea taarifa au ankara husika. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekaidi,” amesema Mwamsojo.

Kamishna huyo amesema ili kuhakikisha ukusanyaji unaimarika, ofisi hiyo imeweka mikakati mbalimbali, ikiwemo kusambaza ankara kwa wadaiwa wakubwa 100 katika kila halmashauri. Kundi hilo linatajwa kuchangia zaidi ya asilimia 89.53 ya deni lote la kodi ya pango la ardhi mkoani humo, ambapo jumla ya wadaiwa ni 119,783.

Aidha, kwa kushirikiana Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), ofisi hiyo inapanga kusambaza ankara za madai zenye thamani ya Sh428.8 milioni kwa wawekezaji wanaodaiwa, huku juhudi zikielekezwa kwenye maeneo yenye shughuli za kiuchumi kama vituo vya mafuta, viwanda na biashara nyingine.

Mbali na hilo, matumizi ya teknolojia pia yamepewa kipaumbele, na wadaiwa watakuwa wakipokea ujumbe mfupi wa simu (SMS) kama njia ya kuwakumbusha kulipa kodi hiyo kwa wakati.

Akizungumzia sheria ya kodi ya pango la ardhi, Ofisa Ardhi wa Jiji la Dodoma, Matilda Mactavo, amesema kodi hiyo ni moja ya vyanzo muhimu vya mapato ya Serikali inayotozwa kwa wamiliki wote wa ardhi wenye hatimiliki nchini Tanzania.

Kodi hiyo inalipwa kwa mujibu wa masharti ya umiliki wa ardhi na imeainishwa kisheria chini ya Kifungu cha 35 cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113.

Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, kila mmiliki wa ardhi anatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka kama sehemu ya masharti ya kuendelea kumiliki ardhi husika.

“Kisheria, kushindwa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ni ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi na kunaweza kusababisha hatua mbalimbali kuchukuliwa dhidi ya mmiliki. Hatua hizo ni pamoja na kutozwa riba au adhabu, kufikishwa mahakamani, na katika hali mbaya zaidi, kubatilishiwa hatimiliki ya ardhi,” amesema

Amesema sheria pia inatoa mamlaka kwa Wizara inayosimamia ardhi kuhakikisha ukusanyaji wa kodi hiyo unafanyika kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kutoa notisi, kusambaza ankara na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa sugu.

Ofisa ardhi huyo amesema umuhimu wa kodi ya pango la ardhi hauishii tu kwenye kuongeza mapato ya Serikali, bali pia husaidia katika usimamizi bora wa ardhi, kudhibiti matumizi holela ya ardhi na kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inatumika kwa tija kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Hivyo, msisitizo unaotolewa na Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Dodoma ni sehemu ya utekelezaji wa sheria na sera za Serikali zinazolenga kuhakikisha kila mmiliki wa ardhi anatimiza wajibu wake kwa wakati, ili kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *