Tabora. Wamiliki wa viwanja na ardhi mkoani Tabora wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi wamepewa siku 14 kulipa madeni yao, huku Serikali ikionya hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokaidi agizo hilo.

Agizo hilo limetolewa Mei 5, 2026 na Mratibu wa Kodi ya Pango la Ardhi na Makusanyo Mengine mkoa wa Tabora, Daniel Boke, wakati wa zoezi la ukaguzi, uhakiki na usambazaji wa ilani kwa wadaiwa wenye malimbikizo ya kodi.

Boke amesema zoezi hilo linalenga kuwabaini wadaiwa sugu na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa hakuna atakayevumiliwa.

“Tunaendelea na ukaguzi kuwabaini wadaiwa, lakini mkazo mkubwa uko kwa wale wenye malimbikizo makubwa kuhakikisha wanalipa. Hili tutalisimamia kikamilifu,” amesema.

Amesema baada ya muda wa siku 14 kumalizika, Serikali haitasita kuchukua hatua ikiwemo kuwafikisha wadaiwa mahakamani au kufuta umiliki wa viwanja husika kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Boke, hali ya ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi mkoani humo si ya kuridhisha, licha ya kuwepo kwa zaidi ya wamiliki 100,000 wa viwanja.

Amesema hadi sasa mkoa umefanikiwa kukusanya takribani Sh2 bilioni pekee, sawa na asilimia 50 ya lengo la Sh4 bilioni lililowekwa.

“Hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hii. Haiwezekani watu wanamiliki ardhi halali lakini hawalipi kodi yake. Kodi hii ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Aidha, amewaagiza waratibu wa ardhi katika wilaya zote za mkoa huo kuongeza juhudi za uhamasishaji na usimamizi ili kuhakikisha wamiliki wote wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Tabora, Damas Mwakindingo, amesema manispaa hiyo ina zaidi ya viwanja 47,000 vilivyomilikishwa rasmi, lakini ulipaji wa kodi bado ni changamoto kubwa.

Waratibu wa kodi ya pango la Ardhi wakiwa kwenye ukaguzi wa wadaiwa wa kodi hiyo katika manispaa ya Tabora.

“Wamiliki wapo, lakini mwitikio wa kulipa kodi si mzuri. Hata hivyo, sheria itachukua mkondo wake kwa wote watakaokaidi,” amesema.

Baadhi ya wananchi wamekiri changamoto ya uelewa kuhusu kodi hiyo. Morice Michael, mkazi wa Tabora, amesema awali hakuwa akitofautisha kati ya kodi ya jengo na kodi ya pango la ardhi.

“Mimi nilijua ni kodi moja tu. Lakini sasa nimeelewa, nitalipa. Hii ni serikali yetu, kodi ndiyo maendeleo yetu,” amesema.

Naye Kelvin Kayaga amesema elimu zaidi inahitajika kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi hiyo.

“Sio kwamba watu wote wanakataa kulipa, wengine hawana uelewa tu. Serikali iendelee kutoa elimu ili kila mtu ajue wajibu wake,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *