TAARIFA kutoka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wamefanikiwa kukamilisha mazungumzo ya kumuongezea mkataba wa mshambuliaji wao tegemeo, Prince Dube ambaye anatarajiwa kusaini miaka miaka miwili kabla ya msimu wa sasa kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani zinaeleza kuwa, pande zote mbili zimefikia makubaliano kamili, huku kilichobaki kikiwa ni hatua ya mwisho ya kusaini mkataba huo, hatua inayotarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimebainisha kuwa uamuzi wa kumuongezea mkataba Dube umebarikiwa na benchi la ufundi la sasa, likiridhishwa na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi hicho hasa kwenye eneo la ushambuliaji.
“Benchi la ufundi limeridhia kabisa aongezewe mkataba, lakini pia hata namba zake za mabao zimechangia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi huo, kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa ndani ya Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na hilo, rekodi ya Dube katika kufumania nyavu imekuwa moja ya sababu kuu zilizowashawishi viongozi wa Yanga kuendelea kuwa na imani naye, wakiamini bado ana mchango mkubwa katika malengo ya timu hiyo ya ndani na kimataifa.
Pamoja na hatua hiyo, Yanga bado inaendelea kufanya tathmini ya kuongeza mshambuliaji mwingine wa kigeni ili kupanua machaguo ya benchi la ufundi, hasa ikizingatiwa changamoto ya majeraha iliyowakumba msimu huu. Katika msimu huu, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilikumbwa na pigo baada ya wachezaji kadhaa kuumia, akiwemo Clement Mzize, Dube mwenyewe pamoja na Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambao wote hawa wanacheza nafasi hiyo ya ushambuliaji.
Kutokana na hali hiyo, mzigo mkubwa uliangukia kwa Emmanuel Mwanengo ambaye hata hivyo hakuwa na makali, huku eneo la mbele likibebwa na viungo washambuliaji ambao kazi yao ilikuwa kuhakikisha timu inapata ushindi.
Wakati Dube akiwa kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba, taarifa zinadai kwamba, mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe alikuwa na ofa kutoka timu za Morocco na Saudi Arabia zilizoonesha nia ya kutaka huduma yake, baada ya kusikia mkataba wake uko ukingoni. Huu ni msimu wa pili kwa Dube ndani ya Yanga aliyojiunga nayo 2024-2025 akitokea Azam FC. Katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara, matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua aliyekuwa Simba akimaliza na 16. Wakati Clement Mzize wa Yanga akifunga 14.
Msimu huu, Dube amekuwa na moto katika kufumania nyavu akifanikiwa kucheza mechi 16 na kufunga mabao tisa ndani ya Ligi Kuu Bara.