Mkurugenzi wa Mashindano ya Fahari Supercup, Wilbert Mweta, ameiomba serikali kutoa mikopo kwa wadau wanaoendesha mashindano ya michezo katika ngazi za chini ili kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.

Akizungumza jijini Mwanza, Mweta ameiomba serikali kuunga mkono jitihada za wadau wanaoendesha ligi za chini na uboreshwaji wa miundombinu ya kuchezea.

“Serikali itambue uwepo wetu na kutuunga mkono kwa kutupatia mikopo ili itusaidie kuendesha mashindano kama haya kwa kuwanufaisha vijana kupata zawadi kubwa zenye kuwasaidia kuendesha maisha na kutimiza ndoto zao.

“Zawadi kama goli la mama kwa timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, fedha hizo hawazihitaji sana, ila ikiwekwa kwa mashindano kama haya inawaongezea hamasa zaidi vijana,” amesema.

Pia amesema serikali iboreshe miundombinu ya kuchezea kama viwanja kwa kufanya marekebisho ili kuwasaidia vijina kuonyesha uwezo wao na kufanya vizuri katika mashindano.

Fahari Supercup itakayoanza Mei 8, 2026 kwenye Uwanja wa Ngomeni uliopo Kata ya Kisesa jijini Mwanza, itashirikisha timu 32 na kudumu kwa takribani miezi miwili.

Mshindi wa kwanza katika Fahari Supercup atapata Sh2.5 milioni na ngao, huku atakayeshika nafasi ya pili akiondoka na Sh1.5 milioni. Pia kuna zawadi ya Sh100,000 kwa kipa bora, mchezaji bora na mfungaji bora.

Wadhamini wa mashindano hayo kwa upande wao wameeleza kuwa kuunga mkono katika shindalo hili ni muhimu kwani inakuza vipaji vya vijana na kuwaletea mafanikio makubwa katika maisha yao.

Kwa upande wa Kocha wa Kisesa Kwanza, John Buguba, amesema licha ya kuwa hajawahi kushinda katika misimu yote aliyoshiriki, lakini kwa sasa amekuja na nguvu ya kushinda tu.

“Misimu iliyopita wachezaji wetu walikuwa hawajajengeka vizuri, lakini awamu hii ushindi lazima,” amesema kocha huyo.

Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita 2025 wa Fahari Supercup, Tinsela FC iliibuka bingwa kwa kuifunga Mweta U20 mabao 2-1 katika mechi ya fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *