Dar es Salaam. Kampuni ya Perseus Mining imesema uwekezaji mkubwa katika mradi wa dhahabu wa Nyanzaga, Sengerema Mwanza unaotarajiwa kuanza uzalishaji Januari 2027, utachochea fursa za kiuchumi kwa wananchi na Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Craig Jones, akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam amesema mradi huo wenye thamani ya Dola 523 milioni (Sh1.36 trilioni) ni wa kiwango cha kimataifa na unaendelea kujengwa kwa kasi huku ukiwa ndani ya ratiba iliyopangwa.

Jones amesema hatua iliyofikiwa inaashiria mafanikio makubwa katika sekta ya madini nchini.

Amesema mradi huo unatarajiwa kuzalisha dhahabu kwa zaidi ya miaka 16, hali itakayochochea mapato endelevu kwa jamii zinazozunguka mgodi huo pamoja na uchumi wa Taifa kwa jumla.

Aidha, amebainisha uwekezaji huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi.

Jones amesisitiza mkakati wa kampuni unazingatia ulinzi wa mazingira, usalama wa wafanyakazi, ajira kwa Watanzania, pamoja na kuhakikisha manufaa ya haki kwa wadau wote, ikiwamo Serikali na jamii zinazozunguka mradi huo.

Amesema Perseus Mining inamiliki asilimia 80 ya mradi huo, huku Serikali ya Tanzania ikimiliki asilimia 20.

Amesema hadi sasa, ujenzi wa mgodi umefikia takriban nusu, huku Dola 250 milioni (Sh650 bilioni) tayari zimetumika.

Ofisa Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Lee-Anne de Bruin amesema mradi huo umeajiri zaidi ya wafanyakazi na makandarasi 3,000, huku asilimia 97 ni Watanzania.

“Tunatoa kipaumbele kwa ajira na uwezeshaji wa Watanzania, hususan wa maeneo ya karibu, pamoja na kununua bidhaa na huduma kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kukuza uchumi wa ndani,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Perseus Mining, Rick Menell amesisitiza wajibu wa kampuni hiyo katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa uadilifu.

“Rasilimali hizi ni mali ya Tanzania. Tunajiona kuwa wasimamizi wake kwa niaba ya Taifa, hivyo tunahakikisha zinatumika kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” amesema.

Menell ameongeza kuwa kampuni ina mpango wa kuufanya mradi wa Nyanzaga kuwa kituo cha mafunzo ya kiufundi kitakachochangia kuzalisha wataalamu wa baadaye katika sekta ya madini.

  • Isaac Lupokela, Meneja wa mgodi wa Nyanzaga akizungumza katika  hafla ya kuelezea maendeleo ya  uwekezaji wa  mradi wa mgodi wa  Nyanzaga unaotarajiwa kuanza uzalishaji wa dhahabu Januari 2027 Sengerema, Mwanza.

Naye Meneja wa Mradi wa Nyanzaga nchini, Isaac Lupokela amesema mradi huo unaendeshwa kupitia Kampuni ya Sotta Mining Corporation Limited na ubia kati ya Serikali ya Tanzania (asilimia 20) na Perseus Mining (asilimia 80).

Amebainisha sekta ya madini kwa sasa inachangia takriban asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi baada ya kuanza kwa uzalishaji katika mgodi wa Nyanzaga.

“Tumewekeza kiasi kikubwa, na mara tu uzalishaji utakapoanza, mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa utaongezeka zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *