Morogoro. Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania bado wanategemea kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia, hata hivyo, Jeshi la Magereza limeanza kuandika historia mpya baada ya magereza yote 129 nchini kuhamia matumizi ya nishati safi, ikiwemo mkaa mbadala, gesi asilia, LPG na biogas.
Hatua hiyo imekwenda sambamba na usambazaji wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala zenye thamani ya Sh914 milioni, zilizogawiwa katika magereza 21 nchini.
Teknolojia hiyo imetajwa kuwa mkombozi wa mazingira na chanzo kipya cha mapato kwa Jeshi la Magereza pamoja na Taifa kwa ujumla.
Akifungua mafunzo ya matumizi ya mashine hizo mjini Morogoro jana, Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi la Magereza, Chacha Binna, alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhamia matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2050.
Amesema mabaki ya mazao ambayo kwa muda mrefu yalionekana kutokuwa na thamani sasa yanatumika kuzalisha mkaa mbadala, hatua inayopunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa kawaida.
Kamishna wa Fedha na Mipango wa jeshi la magereza Tanzania, Chacha Binna akizungumza wakati wa kuzindua jengo la kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala wa jeshi magereza Kihonda, Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
“Mafunzo haya ni ya kimkakati kwa Jeshi la Magereza na Taifa kwa ujumla, kwa kuwa yanagusa uchumi, mazingira, usalama na utekelezaji wa sera ya matumizi ya nishati safi,” amesema Binna.
Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza ni mzalishaji mkubwa wa mabaki ya mimea kupitia shughuli zake za kilimo na viwanda, hivyo teknolojia hiyo itasaidia kuyageuza mabaki hayo kuwa rasilimali yenye thamani ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Binna, mashine hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mkaa mbadala, kupunguza gharama za nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Aidha, amesema mpango huo utawapa wafungwa stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajiri baada ya kumaliza vifungo vyao.
“Mkaa mbadala unaweza kuwa bidhaa ya biashara na chanzo muhimu cha mapato kwa Jeshi la Magereza na Taifa endapo uzalishaji wake utaongezeka na kusimamiwa vizuri,” amesisitiza.
Kamishna wa Huduma za Urekebu, Amina Kavirondo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo askari na wataalamu wa magereza katika matumizi sahihi ya mashine hizo ili kuongeza ufanisi wa nishati safi ya kupikia.
Amebainisha kuwa matumizi ya mkaa mbadala si tu yanasaidia kuhifadhi mazingira, bali pia ni sehemu ya kuwajengea wafungwa ujuzi wa kujitegemea baada ya kutumikia vifungo vyao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kuja na Kushoka Tools and Manufactures Ltd, Leonard Kushoka, amesema mashine moja ina uwezo wa kuzalisha tani tatu za mkaa mbadala kwa siku, kiwango kinachoweza kuokoa zaidi ya miti 60 isikatwe kila siku.
Ameeleza kuwa tani moja ya mkaa wa kawaida huhitaji zaidi ya tani 12 za miti, huku tani nne za mabaki ya mimea zikitosha kuzalisha tani moja ya mkaa mbadala.
Ameongeza kuwa iwapo teknolojia hiyo itatumika kwa kiwango kikubwa nchini, inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa misitu.
“Kwa sasa Tanzania inapoteza takribani hekta 400,000 za misitu kila mwaka kutokana na uzalishaji wa mkaa, lakini matumizi ya mkaa mbadala yanaweza kuokoa zaidi ya hekta 300,000,” amesema.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Sajenti Shida Mkanga kutoka Gereza la Manyoni mkoani Singida amesema elimu hiyo itawasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mkaa mbadala na kuwafundisha wafungwa kutumia teknolojia hiyo kama njia ya kujiajiri baada ya vifungo vyao.
Kwa ujumla, teknolojia hiyo inalenga kulinda mazingira, kupunguza gharama za nishati na kuwajengea wafungwa ujuzi wa kujitegemea.