Marekani. Mtayarishaji wa filamu kutoka nchini India, Karan Johar ameandika historia kama mkurugenzi wa kwanza wa filamu kutoka nchini humo kuhudhuria Met Gala huku vazi lake likivutia macho ya wengi.
Vazi la mtayarishaji huyo lilibuniwa na fashion designer mkubwa kutoka India, Manish Malhotra akisaidiana na Eka Lakhani na kupendezeshwa na michoro ya karne ya 19 kutoka kwa Raja Ravi Varma, jambo lililoipa thamani vazi hilo.
Kwa mujibu wa Karan wakati akifanya mahojiano na Vogue alieleza kuwa vazi hilo halikukamilika kwa mafundi hao watatu bali lilihusisha zaidi ya mafundi 50 na kuchukuwa takribani siku 86 kukamilika.
Hatua hiyo imefanya vazi hilo kutumia takribani saa 5600 kukamilika huku ukitajwa kuwa huwenda ukawa mradi mkubwa wa kibunifu wa mitindo uliyooneshwa Met Gala 2026.
Vazi hilo halikuwa la kawaida, kwani lilitengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu uliyochanganya sanaa ya uchoraji na ufundi wa mitindo ya kisasa. Ambapo lilipakwa rangi pamoja na mafuta kwa mikono ili kuipa michoro mwonekano halisi wa kung’aa.
Pia vazi hilo lilifumwa kwa kutumia nyuzi halisi za dhahabu na ili kufanya lionekane la kisasa zaidi maua ya lotus na swan yalitengenezwa kwa namna ya 3D ili liweze kuonekana kama sanamu ndogo zilizowekwa kwenye kitambaa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagrma Karan ametoa shukrani kwa Manish Malhotra pamoja na Raja Ravi Varma kwa kumtengenezea vazi bora lililoitambulisha India Kimataifa.
“Kuanzia kupenda sinema na mavazi kwenye ndoto tangu nilipokuwa mdogo hadi sasa mkubwa nimesimama kwenye ngazi za The Met Gala… maisha kweli huzunguka na kurudi kwenye mwanzo wake kwa njia zisizotarajiwa sana. Wakati huu haukuwa tu kuhusu mitindo kwangu. Ulikuwa kuhusu kusimulia hadithi.
“Kuhusu kuchukua urithi wa Raja Ravi Varma na kuufanya uishi tena… safari hii si kwa ajili ya picha ya ukutani bali ni kitu kilichovaliwa kwa ajili ya kuiwakilisha India na utamaduni wetu, sanaa yetu na namna yetu ya kusimulia hadithi kwenye ngazi za kimataifa,” aliandika Mtayarishaji wa filamu Karan Johar.
Aidha aliongeza kwa kuandika “Miaka thelathini ya urafiki na ushirikiano na Manish Malhotra na bado tunaendelea kuunda “firsts” pamoja, nakushukuru sana wewe na timu yako kwa kumbukumbu hii ya kipekee kabisa (core memory).”
Met Gala ni tukio la mitindo linalofanyika kila mwaka Jumatatu ya kwanza ya mwezi Mei, lengo kuu la tukio hilo likiwa ni kukusanya fedha kwa ajili ya jumba la makumbusho la The Costume Institute. Ambapo mapato yake husaidia maonesho, machapisho, ununuzi wa vitu vipya pamoja na uendeshaji wa kila siku katika makumbusho hiyo.
Mwaka 2026 tukio hilo lilivutia wengi huku likuhudhuliwa na mastaa wakubwa akiwamo Beyoncé ambaye alirudi tena baada ya miaka 10, Nicole Kidman, Venus Williams, Zoë Kravitz, Sabrina Carpenter, Doja Cat.
Gwendoline Christie, Alex Consani, Misty Copeland, Elizabeth Debicki, Lena Dunham, Paloma Elsesser, LISA, Chloe Malle, Sam Smith, Teyana Taylor, Lauren Wasser, Anna Weyant, A’ja Wilson, Yseult, Adut Akech, Angela Bassett, Sinéad Burke, Rebecca Hall, Aimee Mullins, Amy Sherald na Chase Sui Wonders.
Kwa upande wa India, waliofanikiwa kukanyaga ngazi hizo adimu ni pamoja na Manish Malhotra, Isha Ambani, Karan Johar, Natasha Poonawalla na Ananya Birla.