
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limekamata jumla ya watuhumiwa 209 katika operesheni na misako mbalimbali iliyolenga kuimarisha usalama wa raia na mali kati ya Aprili 1 hadi Aprili 30, 2026.
Jeshi hilo linaendelea kushirikiana na jamii katika kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 6, 2026 na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Rufiji, Protas Mutayoba, watuhumiwa waliokamatwa ni wanaume 118 na wanawake 21.
Amesema watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali, yakiwemo wizi, uvunjaji wa nyumba na maduka, kupatikana na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, wizi wa mifugo, kuingia kwenye hifadhi bila kibali, ubakaji, kupatikana na bangi, pombe haramu ya moshi (gongo), pamoja na makosa ya usalama barabarani.
Katika operesheni hizo, watuhumiwa 36 walikamatwa wakiwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, watuhumiwa 11 walikamatwa na pikipiki 13, na wengine 13 walikutwa na televisheni 12 za aina tofauti ambazo ziliibiwa ndani ya Mkoa wa Kipolisi Rufiji.
Amesema watuhumiwa wengine walikamatwa wakiwa na simu janja sita, simu za kawaida sita, magodoro mawili ya futi 5×6, nondo tano, laptop moja aina ya Dell, mtungi wa gesi, redio mbili, pamoja na vitanda viwili vya kulalia.
Katika eneo la Kisemvule, Wilaya ya Mkuranga, Aprili 18, 2026 saa 12:00 jioni, Jeshi hilo lilikamata nondo 525 za milimita nane na nondo 33 za milimita 12 zenye urefu wa futi 40 kila moja, zilizokutwa katika duka la Victor Yusuph Mande.
“Nondo hizo zilikutwa katika duka hilo baada ya askari kufika dukani kwake; hakuwepo na alizima simu yake baada ya kugundua anatafutwa na Jeshi la Polisi,” amesema Mutayoba.
Amesema nondo hizo zinahusishwa na wizi uliotokea Machi 20, 2026, Njia Panda Kibamba Mwanambaya, ambapo zilikuwa zinasafirishwa kutoka Kibaha kwenda mkoani Mtwara.
“Nondo hizo zimehifadhiwa na upelelezi unaendelea kuhusu tukio hilo,” amesema.
Katika Wilaya ya Kibiti, watuhumiwa watatu walikamatwa kwa wizi wa mifuko 262 ya kemikali aina ya samba sulphur kwa ajili ya zao la korosho, mali ya Correcu Kibiti yenye thamani ya Sh17 milioni.
Mbali na tukio hilo, Mutayoba amesema katika Wilaya ya Mkuranga, Aprili 20, 2026, watuhumiwa nane walikamatwa kwa wizi wa waya za fensi rola saba, mali ya kiwanda cha TANUK cha Kisemvule, zenye thamani ya Sh18 milioni, na watuhumiwa walikiri kuziuza eneo la Tazara jijini Dar es Salaam.
Katika operesheni dhidi ya dawa za kulevya, amesema kilo 26 na gramu 845 za bangi zilikamatwa, huku watuhumiwa 57 wakifikishwa mahakamani na baadhi yao wamehukumiwa vifungo.
“Pia katika kipindi hicho tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 38 wakiwa na lita 38 za pombe haramu ya moshi (gongo) na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria zaidi,” amesema.
Kuhusu mafanikio, amesema jumla ya watuhumiwa 49 walihukumiwa vifungo gerezani na wengine kulipa faini kulingana na uzito wa kosa.
Miongoni mwa makosa hayo amesema ni ubakaji, wizi, uvunjaji, shambulio, uzembe, ukorofi, pamoja na kupatikana na mali za wizi.
Usalama barabarani na elimu kwa jamii
Upande wa usalama barabarani, polisi wameendelea kutoa elimu kwa madereva, wamiliki wa vyombo vya moto na wananchi, hasa katika maeneo ya shule na barabara kuu.
Madereva wanne walikamatwa kwa mwendo wa kasi na kufutiwa madaraja ya leseni, na wengine kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
“Jeshi la Polisi kupitia askari kata linaendelea kutoa elimu mashuleni, nyumba za ibada na majukwaa mbalimbali kuhusu kuzuia uhalifu na ukatili wa kijinsia na watoto katika jamii zinazowazunguka,” amesema Mutayoba.
Kamanda Mutayoba amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuimarisha usalama wa raia na mali.