Dar es Salaam. Wakati makali ya bei za mafuta ya petroli, dizeli na taa yakiendelea kung’ata nchini, hali imezidi kuwa mbaya kwa wananchi kutokana na kupanda kwa nauli, huku upatikanaji wa usafiri wa umma ukiwa wa tabu.

Wengine wameanza kuona magari binafsi kama mzigo, huku wakianza kuangalia namna ya kukabiliana na hali hiyo kupitia usafiri wa umma ili kwenda katika baadhi ya mizunguko yao, huku watumiaji wa magari ya gesi na umeme wakicheka.

Haya yanatokea wakati ambao Serikali imeweka ruzuku ya Sh259 kwa kila lita moja ya dizeli ili kupunguza makali ya bei kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kijamii, zikiwemo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma.

Licha ya hilo kufanyika, Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) kimetaka kuondolewa ulazima wa kuingia kila stendi na ushuru unaotozwa ili kupunguza gharama za uendeshaji, kwani ruzuku iliyotolewa haitazuia bei ya mafuta kuongezeka.

Hata hivyo, wakati petroli na dizeli zikiwa na ongezeko la chini ya Sh500 kwa kila lita, watumiaji wa mafuta ya taa nchini wataumia zaidi kwani kumekuwa na ongezeko la Sh993 kwa kila lita.

Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazoshuhudia athari hasi kupitia ongezeko la bei za mafuta kufuatia vita inayoendelea Mashariki ya Kati, ambayo imepelekea mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafishaji wa mafuta, ikiwemo visima vya uzalishaji, maghala ya kuhifadhi na viwanda vya kusafisha mafuta, na hivyo kuathiri uwezo wa uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo, sasa bei ya mafuta ya petroli ndani ya jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh295 hadi kufikia Sh4,115 kwa rejareja kutoka Sh3,820 iliyokuwapo Aprili mwaka huu.

Mafuta ya dizeli ndani ya jiji la Dar es Salaam sasa yanapatikana kwa Sh4,248 kwa lita moja kutoka Sh3,806 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh442.

Kwa upande wa mafuta ya taa, sasa yatanunuliwa kwa Sh4,677 kutoka Sh3,684 iliyokuwa ikitumika Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh993.

Kwa upande wa watumiaji wa mafuta ya petroli yanayopitia katika bandari ya Tanga, nao wataugulia maumivu kama wenzao, kwani sasa lita moja itauzwa kwa Sh4,176 kutoka Sh3,881, ikiwa ni ongezeko la Sh295 kwa kila lita.

Wanaotumia mafuta ya dizeli yanayopita katika bandari hiyo sasa watanunua lita moja kwa Sh4,309 kutoka Sh3,867 Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh442 kwa lita.

Wale wa mafuta ya taa nao watalazimika kuongeza Sh993 kwa kila lita baada ya mafuta kufikia Sh4,738 kutoka Sh3,745 iliyokuwapo Machi mwaka huu.

Wakazi wa Mtwara watatumia Sh4,207 kununua lita moja ya mafuta kutoka Sh3,912 iliyokuwa ikitumika Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh295.

Mafuta ya dizeli nayo yamefikia Sh4,341 kutoka Sh3,898 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh443, huku mafuta ya taa yakifikia Sh4,770 kwa lita kutoka Sh3,777 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la Sh993.

“Kwa kuwa Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka nchi za Mashariki ya Kati, athari za mabadiliko hayo ya kimataifa zimejitokeza moja kwa moja katika soko la ndani. Ongezeko la bei linaakisi mwenendo wa soko la dunia ambapo bei za mafuta na gharama za usafirishaji zimekuwa zikiongezeka kufuatia athari za vita hiyo,” imesema taarifa hiyo.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini muda wote na kuendelea kuhakikisha bei zinaendelea kuwa himilivu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo zile za kiuchumi na kijamii.

Haya yote yanashuhudiwa wakati ambapo bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la Kiarabu ziliongezeka kwa asilimia 71, 117 na 122 Aprili mwaka huu kutoka wastani wa dola 71.76 za Marekani kwa pipa, dola 85.99 kwa pipa na dola 85.34 kwa pipa Februari mwaka huu kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, mtawalia.

Wamiliki wa mabasi

Katibu wa Taboa, Priscus John, amesema licha ya Serikali kutoa ruzuku katika kila lita ya mafuta, kiwango kilichotolewa ni kidogo ukilinganisha na ongezeko.

“Tunashukuru kwa hiki kidogo, japokuwa tulitegemea ruzuku ikiwekwa ishushwe gharama za mafuta, lakini bado imeendelea kuwa juu, bei inabaki kuwa kubwa. Kwa mazingira ya biashara bado hali inaendelea kuwa ngumu, japokuwa juzi tu tumeongezewa nauli,” amesema.

Amesema ili kupunguza makali ni vyema Serikali iangalie namna ya kuondoa vitu vinavyoweza kupunguza gharama za uendeshaji, ikiwa ni baada ya kuondoa ulazima wa kupita mizani, sasa ligeukiwe suala la stendi.

“Serikali iangalie vitu vingine vinavyoongeza gharama, ikiwemo kulazimishana kuingia kila stendi. Pia ushuru wa kila stendi uangaliwe. Tuangalie vilivyo ndani ya uwezo wetu ili kupunguza mzigo wa gharama; vilivyo nje ya uwezo wetu, kama vita, tuachane navyo,” amesema.

Katika suala la ruzuku, mchambuzi wa uchumi, Dk Lutengano Mwinuka, amesema japokuwa imewekwa kidogo, lakini itasaidia kupunguza mfumuko wa bei usiwe mkubwa sana ukilinganisha na kama isingewekwa.

“Kwa kiasi gani hatujui, lakini itasaidia kudhibiti mfumuko wa bei kwa sababu dizeli ndiyo inayotumika katika magari makubwa, ikiwemo kusafirisha bidhaa kutoka mashambani kwenda sokoni,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam, wamelazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu kufuatia uhaba wa usafiri uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta, hali iliyozua usumbufu mkubwa kwa abiria.

Akizungumza na Mwananchi Jumatano, Mei 6, 2026, mkazi wa Tabata Magengeni, Yasinta Paulo, amesema baada ya kuona hakuna magari na yanayopita yamejaa, walikubaliana na wenzake kutembea hadi watakapopata usafiri.

Amesema jambo hilo si la kawaida kwa upande wao kwani walifika kituoni saa 11 alfajiri ili kuwahi eneo lao la biashara, lakini hawakupata usafiri hadi walipolazimika kutembea hadi eneo la Mwananchi.

“Leo asubuhi tumepata changamoto ya usafiri, tumefika kituoni mapema na ni muda wetu wa kila siku, lakini tulikaa kituoni zaidi ya nusu saa hakukuwa na magari na yaliyopita ni machache yakiwa yamejaa, hivyo tukakubaliana kutembea,” amesema Yasinta.

Amesema mmoja anafanya shughuli zake Mwenge alipata usafiri katika kituo cha TOT na gari lilikuwa limejaa.

Daladala zaegeshwa

Dereva wa daladala, Ali Bakari, amesema baadhi yao wamelazimika kuegesha magari kutokana na changamoto ya gharama za mafuta na masharti ya mabosi wao.

“Baadhi ya madereva wameshindwa kuamsha leo kutokana na maelekezo ya mabosi zao. Wengine wanataka kuongeza kiwango cha kupeleka pesa ya tajiri, mambo ni magumu kwa kweli,” amesema.

Gharama juu magari ya shule

Hali hiyo pia imewaathiri wazazi wanaowapeleka watoto shule kwa kutumia magari ya shule (school bus), wakilalamikia kupanda kwa gharama za usafiri.

“Tulikuwa tunalipishwa kulingana na umbali, na aliyekuwa anakaa umbali mfupi alikuwa analipa Sh50,000, lakini kwa sasa ni Sh70,000 kwa mwezi kwa wanaokaa Tabata. Tunapoelekea, usafiri utaanza kulingana na ada ya muhula wa kwanza, na hii kila mzazi analipa kulingana na umbali anaoishi mtoto,” amesema Antonia Komba.

Huko jijini Mbeya, madereva wa bajaji na bodaboda wameingiwa na hofu ya kuyumba kiuchumi kutokana na kukosekana kwa abiria wa uhakika kufuatia ongezeko la bei.

“Hatujui tunaenda wapi nchi yetu, licha ya jitihada mbalimbali za Serikali, ikiwemo kuwatia moyo Watanzania uwepo wa akiba ya mafuta miezi sita ijayo, jambo ambalo tunaona kigugumizi,” amesema Erasto Mwakalonge.

Mwakalonge amesema kutokana na mtikisiko huo wanapata hofu ya kulazimika kufungia vyombo vya moto ndani kusubiri hali itengamae ndipo waingie barabarani.

“Kimsingi hali ni mbaya. Awali bei za mafuta zilipopaa tulipandisha nauli za usafirishaji abiria kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000 na Sh4,500, kulingana na umbali, licha wananchi kukimbilia kwenye bajaji zenye gharama nafuu,” amesema.

Dereva wa bajaji, Petro John, amesema hali ni ngumu barabarani na kikwazo kikubwa ni kwamba idadi kubwa ya madereva wa bajaji wamepewa mikataba ya marejesho ya kila siku.

“Tuombe Serikali ilitupie jicho suala hilo la mafuta ili kupata mwarobaini wa kudumu kwa kutambua athari za kiuchumi, lakini wapo wafanyabiashara, wafanyakazi na wanafunzi ambao lazima watumie usafiri wa umma kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” amesema.

Habari hii imeandikwa na Aurea Simtowe, Devotha Kihwelo (Dar) na Hawa Mathias (Mbeya)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *